ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, October 6, 2020
SAMATTA ATUA KUONGEZA MZUKA STARS
Na WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM, MTANZANIA
KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kimeingia kambini jana, huku nahodha wa kikosi hicho Mbwana Samatta, akitarajiwa kuwasili leo kuungana na wenzake.
Stars inajiandaa na mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya Burundi, utakaochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Samatta anawasili akiwa ametoka kuipa ushindi timu yake mpya ya Fenerbahçe, iliyoshinda 2-1 juzi dhidi ya Fatih Karagumruk katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uturuki, aliofunga mabao yote mawili.
Wachezaji wengine wanaotoka nje ya nchi walioitwa katika kikosi cha Stars, ni Simon Msuva na Nickson Kibabage, wanatarajiwa kuwasili kesho wakitokea El Jadida, Morocco.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, Clifford Ndimbo, Thomas Ulimwengu anayechezea TP Mazembe ya DR Congo na Ally Msengi kutoka Afrika Kusini, tayari wamefika.
“Timu imeingia kambini leo (jana), nahodha Mbwana Samatta, natarajia kuwasili kesho alfajiri(leo), Himid Mao atawasili Jumatano,” alisema Ndimbo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije, alisema mazoezi yataanza rasmi leo jioni kwenye Uwanja wa Mkapa.
“Wachezaji wote ni wazuri, siku za maandalizi zinatosha kwa sababu wachezaji niliowaita ni wazoefu wanajua majukumu yao na umuhimu wa mchezo huu,” alisema Ndayiragije.
Kocha huyo ameita kikosi cha wachezaji 25, baadhi ya wale wa ndani ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bakari Mwamnyeto, Iddi Mobby, Jonas Mkude, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment