Dar es Salaam
1 Oktoba, 2020
Tamko la Ubalozi wa Marekani kuhusu uchaguzi mkuu ujao nchini Tanzania
Uendeshaji wa chaguzi zijazo nchini Tanzania utakuwa na matokeo muhimu si kwa Tanzania yenyewe pekee, bali pia kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki. Historia ya Tanzania ya kuendesha chaguzi zinazohusisha vyama vingi inarudi nyuma hadi miaka 25 iliyopita na kuifanya nchi hii kuwa mfano wa kuigwa katika bara hili.
Serikali ya Marekani inasisitiza na kuthibitisha kwa dhati kwamba haimuungi mkono mgombea yeyote au chama chochote mahsusi katika chaguzi zijazo za Tanzania. Marekani inaunga mkono mchakato wa kidemokrasia pekee. Tunaunga mkono mchakato wa kweli wa uchaguzi ulio huru, wa haki na wenye uwazi, kabla, wakati na baada ya siku ya uchaguzi. Hii ni pamoja na usalama wa wagombea wote, kuheshimiwa kwa utawala wa sheria, na hali ya mamlaka na vyombo vilivyopewa wajibu wa kusimamia na kuendesha uchaguzi kutokupendelea kabisa upande wowote.
Marekani, pamoja na nchi nyingine za kidemokrasia, itafuatilia kwa karibu matendo ya watu wanaoingilia na kuvuruga mchakato wa kidemokrasia au kuchochea vurugu dhidi ya raia kabla, wakati au baada ya uchaguzi. Hatutasita kufikiria kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaobainika kuhusika katika vurugu na machafuko yanayohusiana na uchaguzi au kukwaza mchakato wa kidemokrasia.
Tunaunga mkono wito uliotolewa na wagombea wakuu wa kuwepo kwa mchakato wa uchaguzi wa amani na wenye uwazi na tunatoa wito kwao na kwa wafuasi wao kuchukua hatua kutanzua hali ya uhasama inayojengeka na kuepuka matamshi ya kichochezi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake