Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi (Kushoto) Dkt. Rashid Tamatamah akiangalia mchoro wa ramani wa majengo matano yanayojengwa kwa ajili ya ofisi za Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika mikoa ya Pwani, Tanga na Lindi, kupitia wizara hiyo chini ya Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH).
Ujenzi wa jengo la ofisi za Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika kata ya Kipumbwi Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga, ambao Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo.
Mratibu wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH) Bw. Nichrous Mlalila (wa kwanza kulia) akimuelezea Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (wa pili kutoka kushoto), namna mkandarasi anayejenga jengo la BMU Kata ya Saadani anavyochelewesha ujenzi huo, hali iliyomlazimu Dkt. Tamatamah kumtaka mkandarasi huyo kukamilisha ujenzi kwa mujibu wa mkataba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga Bw. Oscar Mbenje akimuelezea Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah namna halmashauri hiyo ilivyofanikiwa kukusanya mapato mengi kupitia Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU).
Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika mikoa ya Pwani na Tanga na kubainisha kuridhishwa na ujenzi wa majengo maalum kwa ajili ya ofisi za Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH).
Akizungumza na viongozi wa BMU na wananchi kwa nyakati tofauti mara baada ya kutembelea majengo hayo kwenye Kata ya Dunda Wilaya ya Bagamoyo na Kata ya Saadani Wilaya ya Chalinze katika Mkoa wa Pwani, Kata ya Kipumbwi Wilaya ya Pangani na Kata ya Zingibari Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, Dkt. Tamatamah amesema ujenzi wa majengo hayo unaendelea vizuri huku akiwataka makandarasi kuhakikisha majengo hayo yanakamilika ifikapo mwezi Desemba Mwaka 2020 kama makubaliano yalivyo kwenye mikataba.
“Nimeridhishwa na ujenzi wa baadhi ya majengo hayo kupitia mradi wa SWIOFISH ila ninawaagiza makandarasi kuhakikisha majengo haya yanakamilika kwa wakati ili kuanzia Mwezi Januari Mwaka 2021 yaanze kutumika na viongozi wa BMU kama ofisi katika shughuli mbalimbali za kulinda rasilimali za uvuvi kwenye Ukanda wa Pwani, mkandarasi yeyote ambaye hatakamilisha jengo kwa wakati tutamchukulia hatua.” Amefafanua Dkt. Tamatamah
Ameongeza kuwa mradi huo ambao unahusisha majengo matano ya BMU likiwemo la Kata ya Sudi Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi utakaogharimu zaidi ya Shilingi Milioni 700 ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia, kukamilika kwake kutasaidia kusimamia zaidi rasilimali za uvuvi ikiwa ni pamoja na kutunza nyaraka muhimu.
“BMU zina matatizo ya ofisi na mmekuwa mkishiriki kutokomeza uvuvi haramu, mkikamata nyavu haramu mnaziweka wapi? Ndiyo maana tunawajengea ofisi kupitia mradi wa SWIOFISH. Nia ni ulinzi shirikishi kwa kuwapatia zana, elimu na miundombinu mbalimbali.” Amebainisha Dkt. Tamatamah
Aidha, amesema mara baada makandarasi kukabidhiwa ramani za majengo hayo Mwezi Julai Mwaka 2020 na kutakiwa kuanza mara moja ujenzi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayosimamia mradi wa SWIOFISH kwa upande wa Tanzania Bara inatarajia mara baada ya kukabidhiwa majengo hayo Mwezi Desemba Mwaka 2020, mradi utanunua pia samani na vitendea kazi vingine vya ofisi zikiwemo kompyuta.
Pia, amesema lengo la mradi huo unaotekelezwa katika nchi tatu za Tanzania, Msumbiji na Comoro kwa Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ni kuwajengea uwezo wananchi hususan jamii ya wavuvi kusimamia rasilimali za uvuvi kupitia vikundi, ambapo kwa Zanzibar unasimamiwa na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi hali kadhalika ikiwemo taasisi ya muungano ya Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu (DFSA).
Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku mbili kwenye mradi wa ujenzi wa majengo ya ofisi za Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema mradi huo wa miaka sita ulioanza Mwezi Juni Mwaka 2015 na kutarajiwa kukamilika Mwezi Mei Mwaka 2021, umekuwa ukiendeleza jitihada za serikali ambazo imekuwa ikifanya tangu zamani kwenye maeneo yenye shughuli za uvuvi kote nchini katika kusimamia rasilimali za uvuvi ili kutoa ajira na kuhakikisha mazao ya uvuvi yananufaisha taifa na mwananchi mmoja mmoja.
“Tunatarajia mradi huu kukamilika Mwezi Mei Mwaka 2021 ni mategemeo yetu Benki ya Dunia itaendelea kutupatia mradi huu ambao umekuwa na matokeo chanya katika kulinda rasilimali za uvuvi, pia maeneo ambayo mradi huu bado haujafika nchini, serikali imekuwa ikitenga fedha kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinalindwa kwa kukomesha uvuvi haramu na kutoa elimu juu ya mchango wa seta ya uvuvi kwa jamii ya wavuvi nchini. Amesema Dkt. Tamatamah
Ili kuhakikisha serikali inakusanya mapato mengi kupitia sekta ya uvuvi katibu mkuu huyo amewataka viongozi wa halmashauri nchini kwenye maeneo zilipo shughuli za uvuvi kuvipatia vikundi vya BMU mamlaka ya kukusanya mapato, akibainisha kuwa baadhi ya halmashauri ambazo zimefanya hivyo zimekuwa zikipatiwa makusanyo mengi tofauti na yale ambayo wamekuwa wakikusanya siku za nyuma.
Nao baadhi ya viongozi wa BMU wa maeneo ambayo majengo hayo yanajengwa wamepongeza juhudi za serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kubainisha kuwa mara baada ya kukamilika kwa majengo hayo na hatimaye kukabidhiwa kwa ajili ya ofisi watahakikisha wanayatumia kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kuyatunza ili yadumu kwa muda mrefu.
Wamebainisha kitendo cha kujengewa majengo maalum kwa ajili ya ofisi kuna dhihirisha namna serikali inavyotambua mchango wa BMU katika kuhakikisha wanaisaidia kulinda rasilimali za uvuvi.
Aidha Dkt. Tamatamah amepata pia fursa ya kufika na kukagua nyumba za Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kwenye Hifadhi ya Silikanti Tanga zilizopo Kata ya Kigombe Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, ambazo pia zimejengwa kupitia mradi wa SWIOFISH kwa ajili ya watumishi wa hifadhi hiyo na kuridhishwa na nyumba hizo ambazo tayari zimekabidhiwa wizarani tangu Mwezi Februari Mwaka 2020 na kutaka watumishi watakaotumia nyumba hizo kuzitunza ili ziwe na tija kwao.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amezungumza na jamii ya wavuvi na kusikiliza baadhi ya changamoto zinazowakabili na kuwaahidi kuzifanyia kazi na kwamba wizara imekuwa ikifanya marekebisho ya kanuni na tozo mbalimbali za uvuvi pamoja na kuhakikisha wavuvi wanapata masoko ya mazao yao.
Pia, amewasisitiza akinamama kuendelea na kilimo cha mwani ambacho kimekuwa na tija kwao katika kuendesha familia zao.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake