Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) na Meneja wa Kampuni ya UNIK Construction Company Nchini Tanzania, He Yifeng wakisaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa sh bilioni 70.5 wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini na Butiama.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akibadilishana mkataba wa ujenzi wa mradi wa kupeleka maji kwenye maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini na Butiama na Meneja wa Mkandarasi Kampuni ya UNIK Construction Company, He Yifeng.
Baadhi ya wadau waliohudhuria hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa kupeleka maji kwenye maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini na Butiama. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji wa Wizara ya Maji, Mhandisi Abbas Pyarali.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa tatu kushoto waliokaa) katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na wawakilishi wa Mkandarasi Kampuni ya Kampuni ya UNIK Construction Company mara baada ya kusaini mkataba wa kupeleka maji Butiama na Musoma Vijijini.
Na Mohamed Saif
Serikali imesaini mkataba na Mkandarasi Kampuni ya UNIK Construction Company ya Lesotho kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini na Butiama wenye thamani ya Shilingi Bilioni 70.5.
Akizungumza hapo jana (Novemba 17, 2020) Mkoani Mara wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alisema mradi unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ambao ni Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa. Maendeleo wa Saudia (SFD)
“Mradi tuliosaini leo thamani yake ni Shilingi Bilioni 70.5 na ni fedha za Serikali ya Tanzania; nina kila sababu ya kumshukuru Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea fedha hizi kwa ajili ya kuhakikisha unajengwa,” alisema Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga alibainisha kwamba mradi utajengwa kwa Miezi 24 na alimtaka Mkandarasi kuhakikisha anaukamilisha ndani ya muda huo hasa ikizingatiwa kwamba maandalizi muhimu yamekamilika na hakuna sababu ya kuchelewa.
Alisema kwa kawaida hua baada ya kusaini mkataba mkandarasi anapewa mwezi mmoja kujipanga lakini kwa sasa utaratibu ni kwamba anapaswa kuanza kazi mara moja hasa ikizingatiwa kuwa tayari anaelewa anachostahili kukitekeleza.
“Serikali ya Awamu ya Tano ni ya vitendo, hakuna sababu ya Mkandarasi kutumia mwezi mzima kujipanga kwani tayari hadi hivi anasaini mkataba anaelewa kinachotakiwa kufanywa; maelekezo ya Serikali ni kwamba mradi ukamilike kwa wakati,” alisisitiza Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga alisema katika ujenzi wa miradi, Serikali inazingatia vigezo vikubwa vitatu ambavyo ni ubora, gharama nafuu na muda wa utekelezwaji wake yaani unapaswa ukamilike kwa wakati na hivyo alimtaka Mkandarasi kuhakikisha vigezo hivyo vinazingatiwa.
“Kwa vigezo hivi nilivyovitaja tayari kigezo cha gharama nafuu tumekizingatia na sasa tumebakiza hivyo viwili kwahiyo ninamsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anavizingatia na itakua vyema endapo atakamilisha mradi kabla ya muda huo wa miezi 24,” alielekeza Mhandisi Sanga.
Alisema ujenzi wa mradi ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa wananchi wa Butiama na Musoma Vijijini na kwamba Wizara ya Maji itahakikisha hakuna kikwazo kitakachochelewesha utekelezwaji wake.
“Wananchi wanausubiri kwa hamu kubwa mradi huu kama ambavyo walivyoahidiwa na viongozi wetu, sasa sisi kama Wizara ya Maji katika hili hatutokubali uzembe wa aina yoyote ile, tunachotaka ni kuona unakamilika kwa wakati na kwa ubora utakaoakisi gharama halisi ya fedha itakayotumika,” alisisitiza Mhandisi Sanga na huku akiwataka watendaji wa wizara yake kubaki Mkoani Mara ili kuhakikisha Mkandarasi anakabidhiwa eneo la ujenzi wa mradi ndani ya Saa 24 na kuanza kazi.
Aidha, Mhandisi Sanga alimtaka Mkandarasi kuwapa kipaumbele cha ajira wananchi wa maeneo ya mradi hususan kwenye shughuli ambazo wanazimudu na pia aliwaasa wananchi watakaopata fursa kuhakikisha wanakuwa waadilifu na wanashirikiana na mkandarasi kuulinda mradi.
“Ninaamini zipo shughuli nyingi ambazo wananchi wa maeneo ya mradi wanaweza kufanya hivyo sitarajii kusikia hawapati fursa hizo na pia sitarajii kusikia wananchi wanakwamisha mradi kwa namna yoyote ile,” alisema Mhandisi Sanga.
Mhandisi Sanga aliwakumbusha wananchi kuzingatia maelekezo ya Rais Magufuli ya kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji kwa manufaa yao na kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya UNIK Construction Company Nchini Tanzania, He Yifeng alimhakikishia Mhandisi Sanga kwamba watatekeleza mradi kwa kuzingatia mkataba na maelekezo ya Serikali.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Abbas Pyarali alisema eneo lenye mtandao wa majisafi litaongezeka kufikia asilimia mia moja kwa miji ya Mugango, Kiabakari na Butiama na kwamba zaidi ya wakazi 165,000 watapata huduma ya maji kwa asilimia mia moja.
Mhandisi Pyarali alitaja maeneo yatakayonufaika kwenye awamu ya kwanza ya mradi kuwa ni Miji ya Mugango, Kiabakari, Butiama na vijiji vya Kwibara, Nyamisisye, Kiabakari, Singu, Mwanzaburiga, Kyawazaru, Kamugegi, Kyatungwe, Ryamugabo, Bumangi, Bisarye, Tiring’ati, Butiama, Rwamkoma, Buturu, Nyang’oma, Mayani, Katalyo na Tegeruka.
Halfa ya utiaji saini ilishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Vijijini, Dkt. Vicent Naano na viongozi mbalimbali wa Kata na Vijiji vitakavyonufaika na mradi.
Utiaji saini wa mradi huo mkubwa wa maji ni wa kwanza kutekelezwa tangu kuanza kwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake