Wasanii wa Ngoma Africa toka Morogoro wakicheza jukwani
Wadau wakiangalia onesho la muziki
Na Mwandishi wetu
Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na kikundi cha Ngoma Afrika kilichoko Morogoro imefanya onesho maalum lililobeba ujumbe wa “THAMANI YETU” kwa lengo la kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa thamani Utanzania ili kuienzi na kuidumisha thamani hiyo hasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Jamuhuru ya Muungano wa Tanzania, wabunge, madiwani, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wawakilishi.
Akiwakaribisha wageni mbalimbali walioudhuria onesho hilo kwenye Ukumbi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam, kwaniaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bw Achiles Bufure aliwapongeza Watanzania wote kwa kufanya uchaguzi katika hali ya utulivu na amani hali inayoonesha namna Watanzania wanathamini vyema thamani ya Utanzania wao.
“Misingi iliyojenga thamani yetu ni, Mshikamano wetu, Umoja wetu, Utu wetu, Uzalendo wetu, Amani yetu, Utamaduni wetu, Utajiri unaotokana na rasilimali zetu kama madini, viumbe vya majini na nchii kavu, misitu yetu nk ambapo thamani hii imerithiwa na kusimamiwa vyema na viongozi wetu mbalimbali wa nchi, hivyo hatuna budi kujivunia hata baada ya uchaguzi ndio maana tumeona ni vyema tukawa na onesho hili ili kuwakutanisha watu kwa pamoja kwa lengo la kuimarisha hii thamani tuliyo nayo”. Alisisitiza Bw Bufure
Naye Mkurugenzi wa Ngoma Afrika kutoka Morogoro, Bw Davie Kitururu amesema wamefurahishwa sana kupata nafasi ya kushiriki kwenye onesho hilo lililoandaliwa na Makumbusho ya Taifa ili kuufahamisha umma wa Tanzania juu ya thamani yetu kupitia Muziki wa asili, ngoma za asili na maigizo yaliyoendana na ngoma pamoja na nyimbo mbali mbali za asili.
“Watanzania tunaheshimika sana, hasa sisi tunaopata nafasi ya kusafiri kwa ajili ya kufanya maonesho huko Ulaya, Marekani na Asia tunaona namna thamani yetu ilivyo kubwa, watu wakisikia umetoka Tanzania wanaona ndani yako kuna Amani, Umoja, Mshikamano, Upendo, Muungano wetu, hivyo sisi ngoma Afrika tunataka watu wote wajue thamani yetu”. Aliongeza Bw Kitururu.
Akizungumzia onesho Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania, Bw. Adrian Nyangamale aliwapongeza wasanii wa Sanaa za ufundi na jukwaani walioshiriki onesho hilo na kusema kuwa amejifunza mengi kuhusu umuhimu wa amani nchini kwa kuwa alipata nafasi ya kujumuika na watu wengine huku wakifurahia onesho bila wasiwasi wowote.
“ Ona tulivyo furahia, nimekutana pia na marafiki na kuongeza marafiki wapya, tumekula na kuvywa bila wasiwasi, haya ndiyo maisha tunayo yahitaji, nimejiona mimi ni wathamini sana, kwa kweli naipongeza sana Makumbusho ya Taifa kwa kuandaa onesho hili hasa baada tu ya uchaguzi ili kutukutanisha pamoja na kutukumbusha udugu wetu” alimalizia shuhuda huyo.
Makumbusho ya Taifa kupitia Kituo chake cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam, inaendesha program hii ya Sanaa na Wasanii (Museum Art Explosion) ili kutoa nafasi kwa wasanii wa sanaa za ufundi na jukwaani nchini kutumia jukwaa la kisasa (theatre) na kumbi za maonesho kuonesha kazi zao za sanaa kila Ijumaa ya Mwisho wa Mwezi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake