ANGALIA LIVE NEWS
Monday, February 15, 2021
Gikanji afunguka dili lake na Simba
MASHABIKI wa Simba wana kila sababu ya kunenepa zaidi kwa sasa, kwani wakati jana wakikipokea kikosi chao kilichotua jijini Dar es Salaam kutoka DR Congo walipoenda kucheza mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, kiungo wao mpya ambaye amewachanganya kwa kushindwa kujiunga na timu hiyo, Doxa Gikanji amewaongezea mzuka zaidi.
Kiungo huyo Mkongoman amewahakikisha mashabiki wa klabu hiyo kuwa, wasiwe na wasiwasi naye kwani dili lake na Wekundu wa Msimbazi hao halijafanya na kwamba wajiandae kumpokea Juni, kwani anakuja kukinukisha na kuwapa burudani waliyokuwa wakisubiri kutoka kwake.
Mwanaspoti ambalo limekuwapo jijini Kinshasa tangu Simba ilipotua kujiandaa na mchezo huo, limepata nafasi ya kuzungumza na Gikanji aliyekuwa na kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Chan 2021) zilizofanyika nchini Cameroon.
Katika mahojiano hayo maalumu fundi huyo ambaye hajui lugha nyingine yoyote zaidi ya Kifaransa na Kilingala ameweka bayana kilichomzuia kuungana na Simba na dili lake lilivyo kwa sasa na kusisitia anakuja Juni kukinukisha Msimbazi, kwani kila kitu kipo freshi.
HAPO JUNI TU
Gikanji anasema baada ya dili lake kushindikana mara ya kwanza alikubaliana na Simba atakuja kujiunga na timu katika maandalizi ya msimu ujao ambao utakuwa ni mwezi Juni au Julai.
“Nilishamalizana na Simba katika kila kitu kilichobakia ni mimi kuja kujiunga na timu hapo ndio kulikuwa na changamoto iliyonikwamisha,” anasema.
“Baada ya kumaliza hiyo changamoto na mambo mengine naimani mara baada ya msimu wa kimashindano Tanzania kumalizika nitakuwa hapo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya,” anasema Gikanji mwenye umri wa miaka 30 na kuongeza;
“Nimekuwa nakuja hapa kambini kwa Simba siku mbili mfululizo kutokana na viongozi wa timu hii wana ukarimu mkubwa lakini najiona kama nipo sehemu ya kikosi ingawa sijaanza kutumika. Kikubwa kila kitu kimeenda sawa, tusubiri tu muda ufike nitakuja kuanza kazi ambayo wakati huu ilishindikana,” anasema Gikanji aliyenaswa na Mwanaspoti baada ya kuitembelea kambi ya Simba iliyokuwapo Royal Hoteli akitumia usafiri wa gari yake aina Mark X.
DILI LILIVYOKWAMA
Uongozi wa Simba katika usajili wa dirisha dogo ulipeleka jina la Gikanji katika Shirikisho la Soka Tanzani (TFF), ili kuweza kumtumia katika mashindano ya ndani kutokana na yale ya Kimataifa asingeweza kucheza.
Gikanji asingeweza kucheza mashindano ya kimataifa kutokana klabu yake ilishaitumikia katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Gikanji alilimbia Mwanaspoti wakati inatakiwa kuja nchini Tanzania kuanza kazi na Simba ilishindikana kutokana alikuwa katika majukumu ya timu yake ya taifa ya DR Congo katika mashindano ya Chan kule Cameroon.
“Wakati Simba wanaingiza usajili wangu ili niweze kupata nayo vibali nilitakiwa niondoe kwanza jina langu kwenye usajili wa CAF, ambao ulikuwa unatumika katika mashindano ya Chan ili ndio Simba wakamilishe,” anasema.
“Ikaniwia vigumu kuondoa usajili wangu katika timu ya taifa ikanibidi niwaombe Simba na nikaongea nao na tukakubaliana kuwa nitajiunga nao Juni au Julai kabla ya msimu ujao kuanza,” anasema.
GOMES KIBOKO
Katika hatua nyingine kocha wa Simba, Didier Gomes atahusika kwa kiasi kikubwa kwa wakati huu kumfuatilia Gikanji kuona ni mchezaji ambaye anaweza kufuti katika kikosi chake au vinginevyo.
Wakati usajili wa Gikanji unapitishwa katika kikosi cha Simba wakati huo kocha alikuwa Sven Vandenbroeck ambaye hayupo sasa katika timu.
Gikanji anasema wala hana wasiwasi na anaamini katika uwezo wake na mambo yatakwenda vizuri katika kikosi hicho cha Simba.
“Timu zote ambazo nacheza huwa nafanya vizuri mpaka Simba wameamua kunisajili basi kuna jambo wameliona kutoka kwangu naimani hata kwa Gomes litakuwa suala si gumu kwake na nitajiunga katika timu,” inasema Gikanji.
ANAIPENDA SIMBA
Gikanji inasema kuna timu nyingi ambazo zimeonyesha nia ya kutaka huduma yake lakini amevugiwa zaidi na kikosi cha Simba.
“Kabla ya kufanya uamuzi ya kukubali kuja hapa Simba nimewaomba ushauri makocha na wachezaji mbalimbali waliowahi kupiga Tanzania na wa wakanipa majibu mazuri kuhusu timu hiki,” anasema.
“Simba ni timu kubwa ambayo wachezaji wake wanaishi vizuri, wanapenda kupata mafanikio ya mara kwa mara ndio maana baada ya kuyapata yote hayo nikakubali kujiunga nayo.
“Naipenda Simba kwa mambo mengine mengi ndio maana nipo nao hapa Kinshasa tangu wamefika, nilikuja kuwaona uwanjani siku ya mechi na mpaka leo wanaondoka nipo pamoja nao.
“Nimeangalia timu ilivyocheza mechi ushindani upo katika kila eneo ila naimani nitakwenda kufanya vizuri,” anasema Gikanji.
LIGI YA MABINGWA
Simba wamepata ushindi wa bao 1-0, katika mechi ya kwanza ugenini dhidi ya As Vita na watarudi nyumbani kucheza dhidi ya Al Ahly kutokea Misri siku ya Februari 23, katika Ligi ya mabingwa Afrika.
Gikanji anasema kwa jinsi ambavyo amekiona kikosi cha Simba kinaweza kufanya vizuri katika mashindano hayo na wakafuzu wakawa hata na mechi mechi mkononi.
“Unajua kama Simba watacheza kwa kiwango cha namna hii katika mechi za nyumbani watashinda zote na kufikisha pointi 12, ambazo wanakuwa wameshafuzu huku wakibaki na mchezo mmoja mkononi ugenini dhidi ya Al Ahly,” anasema.
“Kama watacheza kwa kiwango cha namna ambavyo wameonyesha katika mechi na As Vita wanaweza kupata pia pointi nyingine ugenini jambo ambalo watakuwa na dalili ya kumaliza katika kundi katika nafasi ya kwanza na kwenda hatua inayofuata.
“Siona namna ambavyo Simba watashindwa kusonga mbele katika robo fainali ya mashindano haya,” anasema Gikanji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment