Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza umuhimu wa Mpango wa Kurasimisha Rasiliamli na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) katika kuleta ukombozi wa kiuchumi na kuondoa migogoro ya ardhi visiwani Zanzibar wakati Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Mpango huo (Hawapo pichani) walipomtembelea Ikulu Jijini Zanzibar leo Februari 11, 2021 na kueleza hatua iliyofikiwa katika urasimishaji ardhi na biashara visiwani humo.
Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) wakifuatilia hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi walipomtembelea Ikulu Jijini Zanzibar na kufanya naye mazungumzo kuhusu hatua iliyofikiwa katika urasimishaji ardhi na biashara visiwani humo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Bi. Immaculata Senje akieleza mikakati ya mpango huo ikiwemo kupima viwanja 5700, kujenga vituo jumuishi vya Biashara vipatavyo 10 katika wilaya mbalimbali za Unguja na Pemba wakati wajumbe wa Kamati hiyo walipomtembelea Ikulu Jijini Zanzibar leo Februari 11, 2021 na kueleza utekelezaji wa Mpango huo tangua kuanza kwa shughuli za urasimishaji visiwani humo.
Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Dkt. Seraphia Mgembe akieleza kuhusu namna wananchi wa Zanibar wanavyounga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuwaletea ukombozi wa kiuchumi ikiwemo kuwezesha urasimishaji ardhi na biashara unaofanywa kupitia MKURABITA.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa kwenye picha ya pamoja na Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Watumishi na Menejimenti ya Mpango huo leo Ikulu Jijini Zanzibar mara baada ya kukutana na Kamati hiyo.
(Picha zote na MAELEZO)
Na Mwandishi Wetu- Unguja
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) una mchango mkubwa katika kujenga uchumi na kuondoa migogoro ya ardhi baada ya urasimishaji.
Ameyasema hayo leo Februari 11, 2021 Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA na Menejimenti ya Mpango huo.
“Nimejulishwa kuwa Mpango huu tangu uanze hapa Zanzibar, tayari shilingi milioni 441
zimetolewa kuwezesha urasimishaji, naahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea
kutoa kipaumbele kwa kutenga bajeti ili kuendekeza kazi hii ya urasimishaji ”,alisisitiza Rais Dkt. Mwinyi
Akifafanua amesema kuwa mpango wa urasimishaji utasaidia wananchi wengi zaidi kupata mitaji ya kukuza biashara na shughuli za uzalishaji.
Aidha, Mhe. Rais Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Mpango huo Bi. Immaculata Senje ikiwemo kuendelea kutenga bajeti ya urasimishaji.
“Mapendekezo yaliyotolewa na Mpango huu ndizo ahadi zangu za uchaguzi kwa wananchi
ikiwemo kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kufanya kazi zao kwa
tija ”,alisisitiza Mhe.Rais Dkt. Mwinyi
Aliongeza kuwa kujengwa kwa vituo jumuishi vya biashara vipatavyo 10 visiwani Zanzibar
kutasadia kuwawezesha wananchi wengi kurasimisha biashara zao na kuondokana na adha ya
urasimu , hii ikiwa ni moja ya ahadi zake wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Akizungumzia ahadi zake kwa wananchi Mhe.Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni pamoja na;
kuwezesha wananchi kupata mitaji ambapo mpango huo unatoa majibu ya changamoto
zinazowakabili wananchi katika sekta ya ardhi na biashara kwa kuwaunganisha na Taasisi za
fedha kupitia hati zao za kumiliki ardhi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA Bi. Immaculata Senje amempongeza
Mhe. Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa kuchaguliwa na wananchi
kwa kura nyingi.
Aliongeza kuwa MKURABITA imepanga kusajili wajasiriamali 1500, kupima viwanja 5700 katika
wilaya za Pemba na Unguja, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa
urasimishaji ardhi na Biashara .
No comments:
Post a Comment