Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na wauguzi viongozi kutoka mikoa yote nchini kwenye mkutano ambao unalengo la kujadili huduma za uuguzi na ukunga na kuweka mikakati ya kuhakikisha kuna ushirikiano katika kusimamia na kutoa huduma za uuguzi na ukunga ngazi zote
Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka wizara ya afya bi. Ziada Sellah akiongea wakati wa mkutano huo
Afisa Muuguzi kutoka hospitali ya Taifa muhimbili-mloganzila akipokea cheti cha kutambua ubunifu katika kuduma ambapo alitengeneza kifaa ambacho kinasaidia watoto wachanga hasa njiti waliozaliwa wakiwa na tatizo la upumuaji
Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma
Wauguzi Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini wametakiwa kuhakikisha wanajadili sababu zinazochangia kuzorota kwa huduma kwa wateja hali ambayo husababisha kuongezeka kwa malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wateja wanaofika kupata huduma za afya kwenye vituo vyao.
Maelekezo hayo yametolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wauguzi viongozi unaofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Gwajima amesema wauguzi ni rasilimali na nguvu kubwa katika sekta ya afya nchini na duniani kwani ni watoa huduma ya afya ambao wako mstari wa mbele katika kutoa huduma wakati wote kwa kuwahudumia wangonjwa na wateja wenye huitaji bila kuchoka.
“Tufike mahali tuwakatae wale wanaosababisha malalamiko kwa wateja, tubadilike,ni wazi kwamba wauguzi na wakunga kwa umoja wenu na kutumia taaluma, ujuzi na weledi wenu mnaweza mkatupa majibu ya kwanini huduma kwa wateja katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini zinakuwa na changamoto kiasi cha kuleta malalamiko kwa baadhi ya wateja wetu”. Alisisitiza
Aliongeza kuwa ili kuweza kutatua changamoto hizo ni vyema kufufuliwa kwa kamati za maadili za wauguzi ili kuweza kukaa pamoja na kujadili malalamiko yanayowakabili na kuzitafutia njia ya kuzitatua.
“Ninyi ndio mnaojua suala zima la utoaji za afya na mtakao fanya sekta ya afya iende mbele ila wapo wachache wenu ambao wanaharibu taaluma hii,kwahiyo mnaweza kuwarekebisha kwani wauguzi mnaaminika hivyo inaonesha umuhimu wenu kwenye sekta hii”. Alisema Dkt. Gwajima
Hata hivyo Waziri huyo aliwataka wauguzi, wakunga na watoa huduma wengine wote katika sekta ya afya kutoa huduma zinazozingatia utu, heshima na upendo kwa wagonjwa kwani wao wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwajali na kuwatunza wagonjwa na kuwahudumia kwa utaalam,weledi , ubunifu na mtazamo chanya kwa kifuata maadili ya taaluma zao na miongozo ya wizara ya afya.
Naye Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah amesema kuwa mkutano huo utajadili ubora wa huduma za kiuguzi na ukunga na mbinu za kuongeza uzalishaji katika sekta ya afya ili kuondoa kushuka kwa viwango vya huduma za uuguzi na ukunga hasa katika maeneo ya kutolea huduma pamoja na kuongeza kujituma na kujitoa zaidi katika utoaji huduma ili kumsaidia muuguzi kumjua kila mgonjwa na kumhudumia ipasavyo.
Aliongeza kwamba mkutano huo utawakumbusha majukumu muhimu katika utendaji kazi hasa kwa kuihakikisha zinasimamiwa kwa ushirikiano katika ngazi zote “tutatumia wasaha huu kujadili changamoto ambazo zimekuwa zikiathiri ubora wa huduma na kuleta malalamiko kwenye jamii hususan suala la uzingatiaji wa utu, heshima, upendo na maadili ili kuimarisha huduma kwa wateja.
Bi. Sellah amesema baada ya mkutano huo wanatarajia kuja na majibu thabiti ili kuweza kutatua changamoto kubwa kwa kuzingatia nchi inaelekea kwenye mpango wa bima ya afya kwa wote.
Wakati huo huo Afisa Muunguzi Mkuu anayesimamia huduma za Uuguzi na Ukunga nchini pamoja na afya ya uzazi wa mama na mtoto kutoka TAMISEMI Bi.Dina Atinda amesema ofisi ya Rais TAMISEMI imepokea maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya afya na kuahidi kuyafanyia kazi kama wasimamizi wa watoa huduma za afya na hivyo kuwataka wauguzi kufanya kazi kwa kufuata maadili na upendo ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja/wagonjwa ili kuepuka malalamiko na hivyo kuwatendea haki wananchi wanaofika kwenye vituo vyao vya huduma za afya.
Kwa upande wa viongozi amewata kusimamia wauguzi katika ngazi zote ili wauguzi waweze kufanya vizuri kwa kufuata maadili na kuelekeza kufufua kamati za maadili na kukaa kwa pamoja kujadili utendaji kazi wao wa kila siku na wale wanaoshindwa basi kuwapeleka kwenye mabaraza ya kitaaluma.
No comments:
Post a Comment