Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya Rushwa ambapo katika taarifa ya taasisi ya utafiti ya kimataifa Transparency international TI inaonyesha Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 117 mwaka 2015 hadi kufikia nafasi ya 94 kwa sasa kati ya nchi 180 Duniani zilizofanyiwa utafiti.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Jijini Dodoma leo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo amesema taasisi hiyo imetoa alama 38/100 kwa nchi ya Tanzania, awali Tanzania ilipata alama 30/100 na kushika nafasi ya 117 kati ya nchi 180 mwaka 2015, na sasa imepanda kwa alama 8 na kuzipita nchi 23 ndani ya miaka 5.
“January 28, 2021 taasisi ya utafiti ya kimataifa ijulikanayo kama Transparency International imetoa taarifa ya hali ya rushwa Duniani kwa mwaka 2020 ambapo Tanzania imeshika nafasi ya 94 kwa kupata alama 38 kati ya nchi 180 Duniani
Matokeo haya ni kulingana na kiashiria cha Corruption Perception index (CPI) kilichoanzishwa mwaka 1995 kwa lengo la kupima hali ya rushwa katika nchi mbalimbali Duniani” amesema.
Amesema kupanda kwa Tanzania katika utafiti huo ni kutokana na dhamira ya Rais Dkt John Pombe Magufuli baada ya kuingia madarakani mwaka 2015 aliweka mkazo mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Umma.
“Mtakumbuka kwamba mwaka 2015 wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani takwimu za Transparency International za kupima hali ya rushwa nchini zilisema kuwa Tanzania tumepata alama 30/100 na kushika nafasi ya 117 kati ya nchi 180” amesema.
Amesema kulingana na takwimu Tanzania imeshika nafasi ya pili kwa jumuiya ya Afrika Mashariki ikitanguliwa na Rwanda iliyopata alama 54/100, huku Tanzania kwa nchi za Jumuiya ya SADC imeshika nafasi ya 7 kati ya nchi 15 ikitanguliwa na Sychelles, Botswana, Mauritius, Namibia,Afrika Kusini, na Lesotho.
Huku taarifa hiyo ikionyesha kidunia Nchi za Denmark na New Zealand zilishika nafasi ya kwanza kidunia kwa kupata alama 88/100 huku Somalia na Sudani Kusini zilishika nafasi ya 180 kwa kupata alama 12/100.
Ametaja sababu zilizopelekea mafakio hayo katika mapambano dhidi ya rushwa kuwa ni pamoja na dhamira ya dhati ya Rais Dkt Magufuli kudhibiti vitendo vya Rushwa, uchepushwaji wa fedha za Umma na matumizi mabaya ya madaraka.
Nyingine ni mabadiliko chanya ya utendaji kazi wa watumishi wa Umma, na mchango wa wadau, wananchi kufichua vitendo hivyo, vyombo vya habari, na chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU.
Amebainisha kuwa tatizo la rushwa hapa nchini licha ya kupungua lakini bado lipo hivyo ili kumaliza kabisa inahitaji wananchi na wadau kushirikiana na TAKUKURU kuhakikisha vitendo hivyo vinafichuliwa, hivyo wananchi waunge mkono juhudi za TAKUKURU katika mapambano hayo.
No comments:
Post a Comment