Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na Wakuu wa Shule za Msingi wanaoshiriki katika Mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Taasisi ya Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani akimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani yanayofanyika katika Taasisi Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo Mkoani Pwani.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Siston Masanja akizungumza na washiriki wa Mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi.
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari wametakiwa kuimarisha huduma za Malezi, Unasihi na Ulinzi kwa mtoto ili kuboresha ustawi wa wanafunzi shuleni.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako mwishoni mwa wiki wakati akifungua Mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi yanayoendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) katika mikoa 26 nchini.
Profesa Ndalichako amesema Serikali ilikwisha elekeza kila shule kuteua mwalimu ambaye atakuwa anafanya jukumu la ulezi, ushauri na unasihi kwa wanafunzi kwa kuwa hata wanafunzi wanakuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kukwamisha ujifunzaji na kuyamudu masomo.
“Unaweza kukuta kwa bahati mbaya kuna mtoto wazazi wake wamepata ajali na kufariki hivyo mwanafunzi kama huyo anapaswa kupewa ushauri na unasihi ili aweze kuyamudu masomo na kumudu janga ambalo limemtokea hapa duniani,” ametolea mfano Profesa Ndalichako.
Waziri Ndalichako amewataka kufungua ofisi hizo na kuhakikisha wanafunzi wanazifahamu ili wanapokuwa na changamoto za kisaikolojia ama kifamilia wajue wapi pa kupata msaada. Amesisitiza kuwa hii itaondoa changamoto hususani kwa mtoto wa kike wakati mwingine wanazipata wakiwa shuleni
Waziri Ndalichako pia amesisitiza walimu hao wanaochaguliwa ni lazima wawe na uwezo wa kuficha siri za watoto hao wenye changamoto na kuwalinda ili kuwafanya waaminiwe na wanafunzi hao.
Akizungumzia mafunzo ya uthibiti ubora wa shule wa ndani kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi amesema mafunzo hayo ni sehemu ya muendelezo wa Serikali wa kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wasimamizi wa elimu nchini ambapo kati ya mwaka 2015 hadi 2020 walimu 121,410 wanaofundisha madarasa ya awali na darasa la kwanza hadi la nne walijengewa uwezo kuhusu mbinu za kufundishia na kujifunzia stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Hivyo amewataka walimu wakuu hao wanapomaliza mafunzo wahakikishe wanafuatilia ufundishaji, ujifunzaji na utekelezaji wa upimaji na tathmini shuleni, kusimamia misingi ya uongozi na utawala bora katika shule ili kuboresha utoaji wa elimu na kukinga jamii ya shule dhidi ya majanga moto.
Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo wa Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Siston Masanja alimweleza Waziri kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kusimamia ubora wa shule na kutekeleza majukumu ya uthibiti ubora wa shule wa ndani kwa kuzingatia viwango vya elimu vilivyobainishwa katika kiunzi cha uthibiti ubora wa shule.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Anani iliyoko mkoani…… Wilson…. amesema mafunzo hayo yamewasaidia sana katika kupata mbinu za kuwasaidia kuthibiti ubora wa shule ambazo zitawawezesha kusimamia kwa umahiri mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji.
No comments:
Post a Comment