ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 5, 2021

WATUMISHI WAASWA KULINDA HISIA ZAO NA HISIA ZA WENGINE KUBORESHA UTENDAJI KAZI

Jesse Mashami mwezeshaji kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania akitoa mafunzo ya utendaji kazi katika utumishi wa umma kwa watumishi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, jijini Dodoma.
Mwezeshaji wa mafunzo ya namna bora ya utendaji kazi katika utumishi wa umma Jesse Mashami akitoa mafunzo hayo kwa watumishi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (hawapo pichani), jijini Dodoma.
Mwezeshaji wa mafunzo ya namna bora ya utendaji kazi katika utumishi wa umma Jesse Mashami akitoa mafunzo hayo kwa watumishi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (hawapo pichani), jijini Dodoma.Kulia ni Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Muda Mfupi, Tafiti na Shauri za Kitaalamu Mhandisi Hesea George.
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakiwa katika mafunzo ya utendaji kazi katika utumishi wa umma yanayotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, jijini Dodoma

Na Faraja Mpina – WMTH

Watumishi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wameaswa kulinda hisia zao na kuheshimu hisia za wengine ili kulinda amani, upendo, ushirikiano na kuongeza uwajibikaji mahali pa kazi na jamii kwa ujumla.

Hayo yamezungumzwa na Mwezeshaji Jesse Mashami, wakati wa mafunzo juu ya utendaji kazi katika utumishi wa umma kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, jijini Dodoma

Mashami amesema kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuthamini kazi walizonazo kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika utendaji wao.

“Linda hisia zako ili zisiathiri tabia na mienendo yako na kusababisha kutenda matukio yasiyostahili mahala pa kazi na kwenye jamii inayokuzunguka”, alizungumza Mashami

Aliongeza kuwa ni muhimu pia kuheshimu hisia za wengine kwa kuheshimu utu wao, kuwa wakarimu pamoja na kutambua na kusifia juhudi za wengine kwasababu kila binadamu ana njaa ya kutambuliwa na kusifiwa na wengine.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Zainab Chaula amewaasa watumishi wa Wizara hiyo kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana kuanzia ndani ya vitengo na idara za Wizara hiyo ili kuongeza ari ya kufanya kazi na utekelezaji wa majukumu unaoridhisha.

“Sisi wote ni watumishi wa Serikali tunajenga nyumba moja, tuache fujo, tutembee pamoja kwa upendo na mshikamano katika kutimiza majukumu yetu kwa manufaa ya nchi na Serikali kwa ujumla”, Dkt. Chaula

Naye Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Muda Mfupi, Tafiti na Shauri za Kitaalamu Mhandisi Hosea George ametoa rai kwa watumishi hao kuhakikisha wanatoa mrejesho kwa wakati ili kusaidia utekelezaji wa majukumu na uendeshaji wa Wizara hiyo.

No comments: