ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 16, 2021

WAZIRI NDUGULILE AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA KATIBU WA UMOJA WA POSTA AFRIKA NAMNA YA KUBORESHA HUDUMA ZA POSTA

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo baina yake na Katibu wa umoja wa Posta Afrika Bw. Younouss Djibrine ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma walipokutana kuzungumzia uboreshaji wa huduma za Posta hapa nchini.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile katikati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo baina yake na Katibu wa umoja wa Posta Afrika Bw. Younouss Djibrine ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma walipokutana kuzungumzia uboreshaji wa huduma za Posta hapa nchini kushoto Katibu Mkuu wizara hiyo Dkt Zainabu Chaula, kulia ni Katibu wa umoja wa posta Afrika bw. Younouss Djibrine.
Katibu wa umoja wa Posta barani Afrika bw. Younouss Djibrine akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya mazungumzo yake na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile katika ofisi za Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma walipokutana kujadili namna bora ya kuboresha huduma za posta hapa nchini.

Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile leo umekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa umoja wa Posta barani Afrika Bw. Younouss Djibrine ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma kwa lengo la kufahamiana na kushirikishana njia ya kuimarisha huduma za posta hapa nchini.

Akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya mazungumzo hayo Dkt Ndugulile amesema lengo Katibu Mkuu Djibrine kufika katika Wizara hiyo ni kufahamiana na kubadilishana mawazo pia kuifahamu Wizara hiyo mpya hapa nchini.

“Wote tunajua makao makuu ya umoja wa posta barani Afrika yapo Jijini Arusha na hii leo amekuja kwa lengo la kufahamiana na kubadilishana mawazo kama mnavyojua Wizara hii ni mpya hivyo amefika kwa lengo kuifahamu vizuri na utendaji kazi wake” amesema Dkt Ndugulile.

Amesema Pamoja na mambo mengine wamekubaliana namna bora ya kuziendesha huduma za posta na changamoto zake na namna ya kuboresha huduma za posta katika kuziendesha kidigitali na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Sayansi na teknolojia.

Aidha amesema kwa sasa kumekuwa na mabadiliko ya mifumo ya mawasiliano ambapo zamani jamii ilikuwa ikiwasiliana kwa njia ya barua lakini sasa njia kuu ya mawasiliano ni simu ambapo inakadiriwa watu milioni 51 wanatumia simu katika mawasiliano hapa nchini.

Amesema wamefanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ndani ya shirika la posta ambapo kwa sasa wamejikita katika kusafirisha vifurushi na biashara mtandao ambapo mtu anaweza kuagiza bidhaa nje ya nchi na akaletewa mpaka alipo na kukabidhiwa bidhaa yake.

Aidha amebainisha kuwa kwa kushirikiana na umoja wa posta Afrika wameanza ujenzi wa makao makuu ya umoja wa posta Afrika yatakalo jengwa katika jiji la Arusha na linatarajiwa kukamilika march 2022 ikiwa ni kutimiza ndoto ya mwalimu Nyerere ambae aliomba makao makuu ya posta Afrika kuwa ni Tanzania.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika Bw. Younouss Djibrine amesema amefika katika Wizara hiyo mpya kuona namna inavyofanyakazi na kusifu utendaji kazi ndani ya shirika na ushirikiano anaopata kutoka kwa viongozi katika utendaji kazi wake.

Pia amesifu kauli mbiu ya hapa kazi tu inayotumiwa na Serikali ya awamu ya tano na kwamba kauli mbiu hiyo inakwenda sambamba na vitendo kwa kuanza kushirikiana katika kujenga makao makuu umoja wa posta barani Afrika jengo litakalo kuwa refu zaidi Mkoani Arusha na Serikali imekuwa ikitoa ushirikiano wa kutosha.

Amesema kukuwa kwa Teknolojia hakujaathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za Posta kwa sababu mara nyingi vifaa kama simu na computer hutumika kuagiza mizigo aidha kutoka nje au ndani ya nchi lakini shughuli za posta husaidia kutoka sehemu moja kwenda nyingine ndani ya nchi na nje ya nchi kumfikishia mteja alipo.

No comments: