Advertisements

Wednesday, March 3, 2021

BODI YA MAZOWA,GALAXY FOOD WAMEINGIA MAKUBALIANO NA SHULE 13 ARUSHA UNYWAJI WA MAZIWA MASHULENI


Bodi ya maziwa imesimamia makubaliano kati Shule za msingi 13 mkoani Arusha na kampuni ya uchakataji wa maziwa ya Galaxy food ya unywaji maziwa shuleni kwa wanafunzi mashuleni ili kujenga afya za watoto ikiwa ni mojawapo ya uboreshaji wa lishe kwa watoto.

Akisoma makubaliano hayo jana mwanasheria wa bodi ya maziwa nchini Edwin Bantukki alisema bodi hiyo ndio inasimamia mkataba huo ambapo itakuwa katikati kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kama mkataba unavyoelekeza.

” Maziwa yatakayouzwa shuleni ni yale yaliyosindikwa kwa ubora na siyo mengine na endapo makubaliano hayo yatakiukwa na shule husika watatakiwa kuilipa kampuni gharama zote za maziwa ambayi tayari walishayatumia kutokana na kuvunja makubaliano hayo ” alisema Bantukki.

Kaimu msajili bodi ya maziwa Tanzania Noely Byamungu alisema mpango wa watoto kunywa maziwa shuleni unatekelezwa kwa asilimia kubwa duniani ambapo alisema zaidi ya watoto mil. 100 wanakunywa maziwa na nchi 39 zinaripoti mpango huo isipokuwa nchi ya Tanzania.

“Sisi kama Tanzania hatupo kwenye mpango huu hivyo ndio tumeanza kwa mkoa wa Arusha kama mfano na nchi nzima itatekeleza mpango huu , na hii ni ili kuhimiza unywaji wa maziwa nchini ” alisema Byamungu.

Mkurugenzi wa Kampuni ya chakula ya Galaxy Irfhan Virjee alisema mpango huo utaongeza idadi ya wanywaji maziwa na kupanua wigo wa biashara katika kampuni hiyo ambapo alisema wanazalisha lita 72000 kwa siku tofauti na awali walipokuwa wakizalisha lita 3000 kwa siku.

Kwa upande wa Kaimu katibu tawala mkoa wa Arusha David Lyamongi aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa kuhimiza unywaji wa maziwa shuleni pamoja na kujiunga katika mpango huo ulioanzishwa lengo likiwa kuboresha lishe kwa watoto.

Shule zilizosaini mkataba huo ni pamoja na Shule ya msingi Leganga,Longido, Meru, pamoja na Shalom huku shule tisa zilizobaki zikitarajiwa kuweka saini ya makubaliano hayo hivi karibuni.

No comments: