ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 25, 2021

CHAMURIHO AAGIZA SEPTEMBA, UWANJA WA NDEGE SONGWE KUKAMILIKA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (Wapili kulia mbele), akielekea kukagua ujenzi wa maeneo ya usalama mwanzo na mwisho wa Uwanja wa ndege wa Songwe, jijini Mbeya, wakati alipofika uwanjani hapo kukagua maendeleo ya mradi huo.
Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Songwe kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mbeya, Mhandisi, Abdallah Mziray, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (Watatu kulia), wakati Waziri huyo alipofika Uwanjani hapo kukagua maendeleo ya ujenzi wake.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi GECI Espanola S.A ya Spain (Wakwanza kushoto), wakati Waziri huyo alipofika Uwanja wa ndege wa Songwe, jijini Mbeya, kukagua maendeleo ya ujenzi wake.
Mkandarasi GECI Espanola S.A ya Spain, akielezea jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, wakati Waziri huyo alipofika Uwanja wa ndege wa Songwe, jijini Mbeya, kukagua maendeleo ya ujenzi wake.
Mafundi wa Kampuni ya GECI Espanola S.A ya Spain, wakiendelea na zoezi la usimikaji wa miundombinu ya taa katika Uwanja wa ndege wa Songwe, jijini Mbeya. Zoezi hilo likikamilika litapelekea ndege kuruka na kutua usiku uwanjani hapo.
Muonekano wa njia ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa ndege wa Songwe, jijini Mbeya.
Muonekano wa Zahanati inayojengwa na Mkandarasi China Railway 15th Group, anayejenga barabara ya Chunya – Makongolosi kwa kiwango cha lami (Km 39), ambapo Mkandarasi huyo aliahidi kujenga Zahanati hiyo ili kurudisha huduma kwa jamii.
Muonekano wa Barabara ya Chunya – Makongolosi kwa kiwango cha lami (Km 39), ambayo inajengwa na Mkandarasi China Railway 15th Group imefika asilimia 87 na inatarajiwa kukamilika mwezi wa Saba mwaka huu.

PICHA NA WUU

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, amemuagiza Mkandarasi GECI Espanola S.A wa Spain anayesimika taa katika uwanja wa ndege wa Songwe, kuhakikisha anakamilisha zoezi hilo ifikapo mwezi wa Tisa mwaka huu, ili kuruhusu ndege kuweza kutua usiku.

Aidha, Waziri Chamuriho ameagiza pia, ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege unaotekelezwa na Mkandarasi M/s China Geo Engineering Corporation katika uwanja huo, nao kukamilika ifikapo mwezi wa Saba mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Waziri Chamuriho amebaini kuwa Makandarasi hao wana uwezo wa kukamilisha kazi zilizobaki katika miezi hiyo ili sasa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani kuweza kufurahia huduma za usafiri wa anga mchana na usiku kama wengine.

“Mara baada ya kukagua uwanja huu, nimebaini kuwa Makandarasi hawa wana uwezo wa kukamilisha kazi hizi mapema, maana vifaa vyote muhimu vinavyotakiwa kwa ajili ya kazi vimeshawasili isipokuwa mashine ya kukwangua lami ambayo inatarajiwa kuwasili mwezi Mei”, amesema Chamuriho.

Chamuriho, amefafanua kuwa adhabu za kimkataba zitatolewa kwa Makandarasi hawa endapo wakishindwa kukamilisha kazi hizo kwa muda walioahidi.

Katika hatua nyingine, Waziri Chamuriho amekagua mradi wa ujenzi wa Barabara ya Chunya – Makongolosi kwa kiwango cha lami (Km 39), ambapo amesema kuwa mradi huo umefika asilimia 87 na kumtaka Mkandarasi China Railway 15th Group kukamilisha ujenzi huo mwezi wa Saba mwaka huu kama alivyoahidi.

Amempongeza Mkandarasi huyo kwa kujenga zahanati yenye jengo la mama na mwana pamoja na jengo la upasuaji ambayo aliahidi kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la barabara hiyo mwezi Mei 2019, ili kurudisha huduma kwa jamii .

Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Songwe, Mhandisi, Abdallah Mziray, amesema kuwa mradi huo ambao unagharimu shilingi Bilioni 14.7 unaendelea vizuri kwani tayari Mkandarasi amekamilisha kazi ya ujenzi wa maeneo ya usalama mwanzo na mwisho wa uwanja (RESA), na kwa sasa anaendelea na matayarisho ya uwekaji wa tabaka la lami.

“Kazi zinaendelea vizuri, ujenzi wa RESA umekamilika, na kwa sasa Mkandarasi ameanza matayarisho kwa ajili ya kusimika taa za kumuongoza rubani wakati wa kutua”, amefafanua Mziray.

Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Peter Mkolwa, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongolosi (Km 39), unaenda sambamba na ujenzi wa zahanati ambapo amebainisha kuwa ujenzi wa barabara hiyo umefika asilimia 87 na Zahanati umefika asilimia 60.

Waziri Chamuriho, amekamilisha ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mbeya ambapo alikagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake ili kujionea maendeleo yake ikiwemo mradi wa ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Songwe na barabara ya Chunya – Makongolosi (Km 39) kwa kiwango cha lami.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

No comments: