ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 25, 2021

NAIBU WAZIRI WAITARA AZITAKA SEKTA ZA UJENZI NA UCHUKUZI KUFANYA KAZI KWA PAMOJA

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akisisitiza jambo kwa menejimenti za taasisi zilizo chini ya Wizara yake (hawapo pichani) katika kikao kazi kilichofanyika mkoani Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa menejimenti za taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wakifatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mwita Waitara (hayupo pichani), mkoani Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Wakala huo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (hayupo pichani), katika kikao kazi mkoani Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo mara baada ya kikao kazi na wakuu hao, mkoani Dar es Salaam.

Imeelezwa kuwa mafanikio katika Sekta za miundombinu ya Ujenzi na Uchukuzi nchini ambayo ndiyo roho ya uchumi wa Taifa yatafikiwa tu endapo watumishi na wadau wote wa sekta hizo watafanya kazi kwa ubunifu, nidhamu na uadilifu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, katika kikao kazi na menejimenti za taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo jijini Dar es Salaam ambapo amesisitiza umuhimu wa kila taasisi kujipima kama zina tija na ufanisi wake katika jamii unaharakisha maendeleo ya nchi.

“Hakikisheni kazi zinazofanyika zinapimika kwa kuzingatia Mpango wa Maendeleo 2020 – 2025 na miongozo ya viongozi wakuu wa Serikali ili huduma bora kwa wananchi ziimarike na kuleta nafuu kwa wananchi”, amesema Waitara.

Ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha kuwa nyumba za makazi zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini zinawanufaisha kwanza watumishi wa umma kabla ya kuzipangisha kwa watu wengine kibiashara ili kuondoa utaratibu wa udalali unaofanya Serikali kupata mapato kidogo na madalali kuzikodisha kwa bei ya juu na hivyo kupata faida binafsi.

Ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), kuhakikisha malalamiko, kero na usumbufu kwa wasafirishaji na abiria vinapatiwa ufumbuzi kwa kuzingatia sheria ili kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki na kukuza sekta ya usafiri nchini.

Kuhusu miundombinu ya barabara na madaraja, Naibu Waziri huyo ameutaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kutengeneza mpango kazi wa miaka mitano mitano unaonesha namna bora ya ujenzi wa madaraja na barabara nchini kote ili kuleta matumaini kwa wananchi na kuhamasisha huduma nyingine za kiuchumi.

Naibu Waziri huyo amesisitiza kwamba mafanikio katika sekta ya ujenzi na uchukuzi yatafikiwa haraka kama watumishi, wakandarasi na wadau wote wanaoshiriki katika miradi ya ujenzi watafanya kazi kwa bidii na kuepuka vitendo vya rushwa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amesisitiza kuwa Wakala huo umejipanga kikamilifu kuhakikisha barabara kuu na za mikoa zinapitika kwa uhakika katika msimu wote wa mvua za masika.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa huduma za usafiri wa abiria na uchukuzi wa mizigo kwa njia ya reli zimeimarika na kazi ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kati ya Dar es Salaam – Morogoro – Makutupora na Isaka hadi Mwanza inaendelea kwa kasi.

Naibu Waziri Waitara yupo katika ziara ya kikazi ya siku nne (4) katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga ambapo pamoja na mambo mengine atagua miradi ya sekta hizo na kuzungumza na watumishi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

No comments: