Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akisisitiza jambo kwa uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), namna ya kusimamia nidhamu na matumizi ya fedha alipokagua upanuzi wa Bandari ya Tanga.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Erick Hamis, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, Mkoani Tanga.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Donald Angaile, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, Flow meter iliyojengwa katika Bandari hiyo
Muonekano wa Flow meter katika Bandari ya Tanga ambao ujenzi wake umekamilika.
Muonekano wa barabara ya Tanga – Pangani (KM 50) inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akisisitiza jambo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Tanga, Mhandisi Alfred Ndumbaro, alipokagua ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani (KM 50) inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani Tanga.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Tanga, Mhandisi Alfred Ndumbaro, akitoa taarifa ya hatua za mradi wa ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani (KM 50) inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara alipokagua maendeleo ya ujenzi huo, Mkoani Tanga.
PICHA NA WUU
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ametoa siku 14 kwa uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kumpa taarifa ya mradi wa upanuzi wa Bandari ya Tanga unaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 500.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Naibu Waziri huyo kutoridhishwa na maelezo ya namna kiasi cha shilingi Bilioni 172 zilivyotumika katika ujenzi wa kuongeza kina katika bandari hiyo ili kuziwezesha meli kubwa kutia nanga.
“Natoa siku 14 niwe nimepata taarifa ya kina kuhusu mradi huu na namna ya mchakato wa kumpata mkandarasi ulivyofanyika, nani alifanya upembuzi yakinifu, nani alishauri kutumiwa kwa hizo fedha, nani walihusika katika usimamizi wa huo mradi na tathimini ya fedha zilivyotumika ili kuiwezesha Serikali kuchukua hatua”, amesisitiza Naibu Waziri Waitara.
Amesema nia ya Serikali ni kuiona Bandari ya Tanga ikifanya kazi katika viwango vya juu na hivyo kuchangia kukuza uchumi wa Taifa na yoyote atakayebainika kukwamisha dhamira hiyo ya Serikali atachukuliwa hatua kali.
Amemtaka Mkurugenzi Mpya wa TPA, kupanga safu yake ya uongozi mapema iwezekanavyo ili kuendana na kasi na matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Amewataka watumishi wa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake kusoma mpango wa Maendeleo ya Taifa wa 2020 – 2025 ili kuweza kujua wanatakiwa wafanyeje na kwa namna gani katika kipindi hicho.
“Fanyeni kazi kwa weledi, acheni majivuno, hudumieni wananchi”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TPA, Bw. Erick Hamis, amesisitiza kwamba taarifa zinazotakiwa zitawasilishwa kwa wakati na miradi inayoendelea katika Bandari ya Tanga itakamilika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kuiwezesha Bandari hiyo kuhudumia tani milioni mbili za shehena toka tani laki saba zinazohudumiwa kwa sasa.
“Tutahakikisha uwepo wa reli na barabara za uhakika katika Mkoa wa Tanga kuelekea mikoa ya Kaskazini na katikati ya nchi kunawezesha bandari hii kufanya kazi kwa ufanisi”, amesema Bw. Hamis.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Waitara amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani (KM 50) kwa kiwango cha lami na kumtaka mkandarasi M/S China Henan International kukamilisha barabara hiyo kwa wakati na Serikali haitakubali visingizio visivyo na tija.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Tanga, Mhandisi Alfred Ndumbaro, amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hiyo na zoezi la kulipa fidia litaanza Mei 03, mwaka huu.
Amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa atamsimamia kikamilifu mkandarasi ili kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa viwango na kukamilika kwa wakati na hivyo kufungua ukanda wa Wilaya ya Pangani.
Naibu Waziri Waitara yupo mkoani Tanga kuendelea na ziara yake ya siku nne ya kukagua miundombinu ya Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi ambapo pamoja na mambo mengine amezungumza na watumishi ili kuwapa muelekeo wa Serikali na kusikiliza hoja zao.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
No comments:
Post a Comment