Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (aliyesimama) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai nchini (hawapo pichani) alipokuwa akifungua rasmi kikao cha Kamati hiyo katika Ukumbi wa katika ukumbi wa mafunzo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto jijini Dar es Salaam, Aprili 23, 2021. Kushoto ni Mhe. Sharmillah Sarwatt, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo.
Washiriki wa kikao wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi.
Mhe. Msajili Mkuu akiwaonyesha Wajumbe kijitabu cha utekelezaji wa Majukumu ya Mahakama kwa mwaka 2020. Ametoa rai kwa Wajumbe wa Kamati hiyo kukisoma na kujua mafanikio, changamoto na mipango mbalimbali ya Mahakama ya Tanzania.
Na Mary Gwera, Mahakama
Wadau wa Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai nchini kila mmoja kwa nafasi yake wametakiwa kusimamia sheria ambazo hazitoi mwanya wa kuwa na mlundikano wa mashauri Mahakamani na msongamano wa mahabusu gerezani.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati hiyo alipokuwa akifungua rasmi kikao chao mwishoni mwa wiki iliyopita, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema kuwa kumekuwa na ucheleweshaji wa upepelezi hali inayosababisha mlundikano wa mashauri na mlundikano wa Mahabusu.
“Bado hatusemwi vizuri kwenye suala la mlundikano wa mashauri unaosababisha msongamano wa mahabusu gerezani kwa sababu mbalimbali kama vile kutokamilika kwa upelelezi kwa wakati, Upatikanaji mashahidi, idadi ndogo ya rasilimali watu kama vile Majaji na Mahakimu,waendesha mashtaka na kadhalika,” alisema Mhe. Chuma.
Alisema kuwa changamoto zilizoainishwa zinaweza kuepukwa iwapo kila mdau atafuata sheria, miongozo na taratibu zilizowekwa ili kuwezesha mchakato wa utoaji haki kufikika kwa wakati na ufanisi.
Msajili Mkuu aliongeza kuwa ili kudhibiti hayo Wadau wote wanatakiwa kuwa na utayari wa kutoa huduma na kuwajibika kila mmoja kwa nafasi yake na kutumia mamlaka tuliyonayo hata pale inabobainika kuwepo mashauri mahakamani yasiyo na tija.
“Kwa mfano kusimamia vifungu vya 91,98,225 vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kwa upande wa waendesha mashtaka na Mahakama. Mamlaka ya Mkuu wa Kituo kutoa adhabu ya faini; kwa mujibu wa kifungu 170 (6) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (the Criminal Procedure Act (Cap 20 RE 2019),” alibainisha.
Asisitiza kuwa kwa mashauri yasiyokuwa na ushahidi wa kutosha, yanatakiwa kuwasilishwa maombi maalumu mahakamani ya kuomba amri ya uangalizi kwa mujibu wa vifungu 70-73 vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (the Criminal Procedure Act (Cap 20 RE 2019).
Kwa upande wa Magereza, Mhe. Chuma alishauri kuwa na Matumizi ya adhabu mbadala ambapo Afisa Ustawi wa Jamii anawajibika kupendekeza adhabu mbadala kwa watuhumiwa waliotiwa hatiani kwa makosa ambayo adhabu husika ni chini ya miaka 3, kama inavyobainishwa katika kifungu 3 (1) cha Sheria: The Community Services Act (Cap. 291 R.E. 2019).
“Hivyo, kupitia kikao hiki ni matarajio yangu mtatoa mapendekezo zaidi yatakayowezesha kuendeleza maboresho ya huduma ya utoaji haki nchini ili wananchi waweze kunufaika na huduma hiyo iliyopo kikatiba,” alisisitiza.
Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai nchini yenye Wajumbe kutoa Mahakama, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Chama cha Mawakili wa kujitegemea Tanganyika (TLS), Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza, TAKUKURU kinalenga kujadili mafanikio na changamoto ya uendeshaji wa mashauri ya jinai na mfumo wa jinai kwa ujumla na kupendekeza namna bora ya kushughulikia mashauri hayo.
No comments:
Post a Comment