Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Tabora, hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.Uzinduzi ulifanyika Mei 8, 2021 Tabora
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama akihutubia wakati wa uzinduzi huo.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akitoa salamu za Wizara yake wakati wa uzinduzi huo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akitoa salamu za wizara yake wakati wa uzinduzi huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe pamoja na viongozi alioambata nao wakionesha kitabu cha Mwongozo wa Uwekezaji kwa Mkoa wa Tabora mara baada ya uzinduzi rasmi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya KilimoTanzania (TADB), Japhet Justine akitoa salamu za ofisi yake wakati wa uzinduzi huo.
Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali wakati wa uzinduzi huo.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe amezindua Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Tabora ulilofanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike ulipo katika Ofisi za mkuu wa mkoa huo tarehe 8 Mei, 2021.
Mwongozo huo umetayarishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na Mkoa chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
“Mwongozo wa uwekezaji ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuzitangaza fursa zilizopo hapa mkoa wa Tabora zipate wawekezaji na kusaidia kuinua hali ya uchumi wa watu wa mkoa huu na Taifa kwa ujumla,”Alisema Waziri Mwambe.
Waziri Mwambe amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo mkubwa wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji utakaoinua uchumi wetu.
“Nimesoma mwongozo kuhusu utajiri na fursa nyingi zilizopo katika mkoa huu zikiwemo za maliasili, madini, mifugo, kilimo cha tumbaku, pamba, alizeti pamoja na shughuli za ujasiriamali mdogo na wa kati hivyo zitumieni kwa tija ya uchumi wa taifa kwa ujumla,”alisisitiza Waziri Mwambe.
Aliongezea kuwa, zipo fursa mpya zinazojitokeza katika mkoa huu ambazo ni pamoja na bomba la mafuta ghafi linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga na kupiti mkoa wa Tabora, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, umeme wa REA, barabara za lami, Maji toka Ziwa Victoria na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo cha aina mbalimbali.
Aidha Waziri alieleza matarajio yake kuhusu hali ya uwekezaji katika mkoa huo ikiwemo, kuona kila mtendaji wa Serikali ataondokana na urasimu, na vikwazo visivyo na tija ambavyo vinawakwaza wawekezaji wanapofika katika mkoa kuwekeza.
Akihitimisha hotuba yake, aliutaka mkoa kuendelea kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji cha Kanda (TIC) kilichopo Kigoma kuanzisha Kituo cha kutolea huduma kwa pamoja (One Top Centre) na kuhakikisha kinakuwa na rasilimali za kutosha.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Utatibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama alisema Mpango huu utawawezesha wakulima hususan vijana kupata pembejeo na masoko ya kuaminika ya bidhaa zao na kuhakikisha wanajikita katika kilimo cha mashamba ya Pamoja.
“Programu ya Kilimo cha Mashamba ya Pamoja (Block Farming) inaratibiwa na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuwawezesha wananchi hususan vijana kufanya kilimo biashara chenye tija na kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo ambapo kupita kilimo cha pamoja vijana watawezeshwa kupata mbolea kwa urahisi, kupata pembejeo za kilimo, kuwekewa utaratibu mzuri na nafuu wa kusafirisha bidhaa zao kutoka shambani hadi sokoni na watawezeshwa kupata masoko ya uhakika ya bidhaa zao,”alisistiza Waziri Mhagama.
Mfumo huu ukisimamiwa vizuri ndio njia sahihi itakayoiwezesha nchi yetu kufanya mapinduzi katika Sekta ya Kilimo. Mfumo huu unachochea matumizi ya teknolojia za kisasa na kuwezesha tija kubwa katika sekta ya kilimo.
Naye Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Philemon Sengati alishukuru hatua muhimu ya uzinduzi wa mwongozo huo, huku akieleza namna mkoa utakavyohakiksha unatekelezwa kwa vitendo na kukiri ni tukio la kihistoria na la heshima kwa mkoa kwa ujumla.
Alifafanua kuwa, uwepo wa mwongozo huo utasaidia kutangaza fursa na vivutio vya uwekezaji ikiwemo ardhi, idadi kubwa ya mifugo takribani milioni 3.7, utalii wa kihistoria, uwepo wa madini na mapori ya akiba pamoja na misitu ya hifadhi inayofaa kwa ufugaji wa nyuki na uvunaji wa mazao ya misitu.
“Zipo sababu nyingi za kuwekeza Tabora ingawa hili la utashi wa kisiasa limechochea kuvutia wawekezaji katika kuhakikisha changamoto na vikwazo vinaondolewa kwa wakati,”alisema Dkt. Sengati
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwakilishi Mkazi wa UNDP hapa nchini, Bi.Christine Musisi alisema UNDP itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi. Alisema UNDP itaendelea kusaidiana na Mikoa katika utekelezaji wa miongozo hii kwa kutoa ushauri wa kitaalam na rasilimali fedha panapohitajika.
“UNDP kwa Kushirikiana na Serikali, Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) zimefanikisha kuandaa miongozo katika mikoa 25 na miongozo hiyo ipo katika hatua mbalimbali na itazinduliwa siku za hivi karibuni,”alisema Musisi
Mawaziri wengine waliohudhuria na kutoa neno ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe.
No comments:
Post a Comment