Mtafiti mwandamizi na Meneja Mradi wa Utafiti wa Panya wa SUA-APOPO Dkt. Georgies Mgode akiwa na mmoja wa Panya hao kwenye Maonesho ya Ubunifu na mashindano ya Kitaifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU 2021) Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa tume ya vyuo vikuu nchini (TCU) Prof. Charles Kihampa (Katikati aliyevaa miwani) akiangalia Panya hao wanavyofanyakazi kwenye banda la SUA lililopo katika maonesho na mashindano ya Kitaifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU 2021) Jijini Dodoma.
Baada ya mafanikkio makubwa ya utafiti wa matumizi ya Panya kwenye kutambua mabomu na vimelea vya kifua kikuu na mambo mengine, Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA wanasema kuna uwezekano mkubwa wa Panya hao kutumika kwenye kutambua maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19.
Hayo yamebainishwa kwenye banda la SUA na Mtafiti mwandamizi na Meneja Mradi wa Utafiti wa Panya wa SUA-APOPO Dkt. Georgies Mgode kwenye Maonesho ya Ubunifu na mashindano ya Kitaifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU 2021) Jijini Dodoma.
“Tunaamini Panya wanaweza kutambua virusi vya Corona na Maambukizi yake kwa ufanisi mkubwa maana tumeshaona mafanikio kwenye Utambuzi wa ugonjwa wa kifua kikuu, kwani kila kimelea kina harufu yake na kila ugonjwa unaosababishwa na vimelea tofauti una harufu yake kwahiyo tunaamini Panya wanaweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa sana”. Alibainisha Dkt. Mgode.
Amesema tayari wameshaandika maandiko ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza kazi ya kufundisha Panya hao na zikipatikana wataanza lakini wanaamini watasaidia hasa kutambua wale watu ambao wana vimelea lakini dalili hazijajitokeza maana ukiweza kutambua ugonjwa kabla dalili hazijajitokeza ni rahisi kuzuia maambukizi kwa haraka zaidi.
“ Hii itakuwa na manufaa makubwa maana vipimo vya Corona kwa sasa ni ghari sana na vinatoka nje ya nchi lakini kwa kutumia Panya itakuwa rahisi na pia itaondoa maumivu makubwa kwa watu wanaopimwa wakati wa kuchukua sampuli ukilinganisha na vifaa vinavyotumiwa sasa kwenye kupima wahisiwa wa wagonjwa wa COVID-19” Alisisitiza Mtafiti huyo Mwandamizi Dkt. Mgode.
Aidha Dkt. Mgode ameeleza kuwa kitendo cha kutambua maambukizi ya awali kabisa kwa watu wenye vimelea ni jambo muhimu kwani litasaidia watu kujilinda lakini pia wale watakaokutwa na vimelea watapatiwa huduma mapema na hivyo kupunguza vifo na kusambaa kwa ugonjwa.
Amesema kuna wanasayansi wengi huko nchi zilizoendelea baada ya kuona mafanikio makubwa ambayo Panya wamefikia walifanya majaribio ya kutumia Pua bandia (electronic Nose) kunusa ili kutambua vimelea lakini hawajafanikiwa kama ambavyo SUA wamefanikiwa kwa kumtumia Panya mwenyewe hivyo wataendelea na Panya kutokana na uwezo wake mkubwa katika kutambua.
Dkt. Mgode ameishukuru Serikali kwa kupitisha matumizi ya teknolojia ya Panya kwenye hospitali zake na kwa makubaliano kuwa majibu Panya yathibitishwe na teknolojia zingine zilizopitishwa kabla ya majibu kutumia hospitalini na imekuwa ikifanyika hivyo na kusaidia watu wengi kubainika na kupona baada ya kupatiwa matibabu akitolea mfano mwaka jana 2020 jumla ya wagonjwa 2014 ambao hawakugundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutumia njia za kawaida za hospitali za vipimo walibainika kwa kutumia Panyabuku.
Dkt. Mgode amesema wanashawishika sasa zaidi baada ya kuona kuwa baadhi ya wale ambao wanashuku matumizi ya Panya kwenye kutambua vimelea vya TB sasa wameanza kujadili namna ya kutumia Mbwa katika kufanya kazi hiyo wakati vyote vinatumia mfumo huohuo katika kutambua.
“Tunaamini kabisa kuwa matokeo bora yanayopatikana hapa Tanzania yataweza kusaidia kushawishi na kubadili mitazamo hasi ya baadhi ya mataifa na wanasayansi wengine ambao hawaamini kwenye matumizi ya Panya na hasa ukizingatia kuwa nchi yetu ya Tanzania inaongoza kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Alifafanua Dkt. Mgode.
Mtafiti huyo amesema kwa sasa tusiangalie ni silaha ipi iliyotumika katika kupata matokeao ya ushindi na ugonjwa utakapotokomea ndipo wengine wataamini kuwa mbinu na teknolojia gani inafanya kazi vizuri.
Mradi wa SUA – APOPO unaofanya tafiti za Panya ulio katika kituo cha Udhibiti wa Viumbe Hai Waharibifu ulianza na utafiti wa Panya kwenye kugundua mabomu yaliyotegwa ardhini na ukawa na mafanikio makubwa kwa kuwatumia kwenye nchi mbalimbali duniani hasa za Msumbiji, Angola na Kambodia. Kutambua vimelea vya kifua kikuu,Kutambua utoroshaji wa nyara za Serikali kama pembe za Ndovu na faru pamoja na magamba ya kakakuona,Utoroshaji wa Miti ya mbao ngumu ambayo ipo hatarini kutoweka kwa magendo mipakani.
No comments:
Post a Comment