Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amewatoa hofu Watumishi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kutokana na hofu iliyotanda miongoni mwao na hivyo kuwahimiza kuendelea kuchapa kazi kama kawaida.
Hatua hiyo inakuja kufuatia kukabidhiwa taarifa ya Kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa fedha pamoja matumizi mabaya ya Rasilimali Watu zinazoikabili TTB
Ametoa rai hiyo Jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB mara baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya uchunguzi wa tuhuma hizo.
Waziri Dkt.Ndumbaro amesema hatua ya maamuzi ya taarifa hiyo yataanza kuchukuliwa mwezi Juni mwaka huu kutokana na sasa kukabiliwa na majukumu mengine.
Amesema mara tu baada ya kuipokea taarifa hiyo naye amemkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.Allan Kijazi kwa ajili ya kuifanyia kazi.
” Nakuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TTB itisha kikao na Watumishi zungumza nao watoe hofu wahimize waendelee kuchapa kazi kama kawaida, kama Wizara tutatoa maamuzi ya haki muda ukifika ” amesisitiza Dkt.Ndumbaro
Amesema majukumu ya msingi ya Bodi hiyo hayatakiwi yasimame yakisubiria hatua za maamuzi ya ripoti hiyo mpaka yatolewe.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Dkt. Ndumbaro amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TTB kumchukulia hatua Mtumishi yeyote ambaye hatatekeleza majukumu yake kwa visingizio vya kusubilia hadi pale maamuzi ya ripoti yatakapotolewa.
Itakumbukwa mnamo tarehe 10 April, 2021 Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt.Damas Ndumbaro alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TTB, DevothaMdachi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha pamoja na matumizi mabaya ya Rasilimali watu zinazoikabili Taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Betrita Lyimo amesema atatekeleza maelekezo hayo ikiwemo kuitisha kikao cha Watumishi wote wa Taasisi hiyo kwa lengo la kuzungumza nao kwa kuwatia moyo na kuwasisitiza Wachape kazi .
No comments:
Post a Comment