Wauguzi walioshiriki maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil wakila kiapo cha wauguzi.
Na Ramadhan Ali Maelezo
Mrajisi wa Vyama visivyo vya kiserikali (NGO) Ahmed Khalid Abdalla amewakumbusha Wauguzi kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani ni adui mkubwa wa haki.
Katika kuhakikisha Wauguzi wanatoa huduma bora na kuongeza ufanisi, amewashauri kutumia fursa zilizopo za masomo kuongeza taaluma ili kuhakikisha Afya na Ustawi wa jamii Zanzibar inaimarika.
Mrajisi wa NGO ameeleza hayo katika maadhimisho ya kilele cha siku ya Wauguzi Duniani zilizofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Amesema Wauguzi kama zilivyo taaluma nyengine za afya, ni watu muhimu katika maendeleo ya nchi na nitegemeo kubwa katika kusaidia kuokoa maisha ya wananchi.
Amewahakikisha waunguzi kuwa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili na kuhakikisha inaimarisha miundombinu, Utaalamu na maslahi bora ili lengo la kutowa huduma nzuri liweze kufikiwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Professa Amina Abdulkadir amesema Taaluma ya Uuguzi Zanzibar imeanza kupiga hatua kwa kuanzisha shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) na taratibu za kuanzisha shahada ya uzamili zimeanza kuchukuliwa.
Amesema lengo la kuanzisha shahada hiyo hapa Zanzibar ni kutowa fursa kubwa zaidi kwa wauguzi kuongeza taaluma baada ya kuonekana nafasi za kujiendeleza kwa masomo hayo nje ya nchi ni chache.
Amewataka wauguzi wa Zanzibar kuimarisha umoja na mshikamano na kuwa mfano bora wa tabia njema na kufuata maadili ya kazi hiyo kama alivyokuwa mwanzalishi wa Taaluma hiyo Duniani Bibi. Florence mzaliwa wa Italy.
Katika risala ya Wauguzi iliyosomwa na Zuwena Ali Salim, wameishauri Serikali kuziangalia changamoto zinazoikabili kada hiyo ikiwemo uhaba wa vitendea kazi na maslahi duni.
No comments:
Post a Comment