Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha
Ufundi Stadi cha wilaya ya Ruangwa katika kijiji cha Nandagala , Juni
7, 2021. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Dkt. Leonard Akwilapo na wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya VETA
nchini, Peter Mabuki.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi
Faraji Magama ambaye ni Mshauri Mwelekezi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha
Ufundi Stadi cha wilaya ya Ruangwa wakati alipofugua ujenzi wa Chuo
hicho katika kijiji cha Nandagala wilayani humo, Juni 7, 2021. Kulia
kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ruangwa katika kijiji cha Nandagala, Juni 7, 2021.
Baadhi ya viongozi na wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Ruangwa katika kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa, Juni 7, 2021.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoshiriki katika ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Ruangwa kulinda fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa kuvitunza vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi ili mradi ukamilike kwa wakati.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Samia Suluhu Hassan ameridhia kutolewa kwa fedha za ujenzi huo hivyo ni lazima zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
Ametoa kauli hiyo leo (Juni 7, 2021) wakati alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi.
“Rais wetu anatupenda ndiyo maana katuletea pesa ambazo lazima tuzilinde, tukinunua vifaa vya ujenzi kama vile, mabati, saruji, mbao na nondo lazima vyote vitumike hapa kwenye ujenzi na kamwe tusiruhusu udokozi”
Pia Waziri Mkuu ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Uongozi wa VETA na Suma JKT kwa kusimamia kwa weledi na uaminifu ujenzi wa chuo hicho na amewataka kuhakikisha kwamba ujenzi unakamilika kwa wakati ili mafunzo yaanze kutolewa.
Akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema chuo hicho kitajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itagharimu shilingi bilioni 2.1 na awamu ya pili itagharimu shilingi bilioni 1.2.
Amesisitiza kuwa mafunzo ya muda mrefu katika chuo hicho yanarajiwa kuanza mwenzi Januari 2022 kwa mujibu wa mafunzo ya VETA.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema kuwa Chuo kitakuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa wakazi wa eneo la Nandagala na wilaya ya Ruangwa hivyo wazazi wawapeleke watoto wao wakajipatie maarifa na ujuzi.
No comments:
Post a Comment