Advertisements

Saturday, June 12, 2021

Mkutano wa G7 waanza nchini Uingereza


Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesifu hatua ya kufanyika kwa mkutano wa ana kwa ana wa viongozi wakuu wa kundi la mataifa tajiri la G7.

Viongozi wa kundi la G7 na wakuu wa Umoja wa Ulaya wakiwa kwenye mazungumzo wakati wa mkutano wa kilele mjini Cornwall.

Mkutano huo unafanyika kwa mara ya kwanza baada ya karibu miaka miwili na Johnson ameutaja kuwa "nafasi muhimu" ya kujiimarisha tena na kulishinda janga la virusi vya corona. 

Akifungua mkutano huo wa kilele wa kundi la G7 unaofanyika katika mji wa pwani wa Cornwall mashariki ya Uingereza, Johnson amesema ni muhimu kwa ulimwengu kulishinda janga la corona kwa kiwango sawa ikiwa lengo ni kuitoa dunia kutoka kwenye madhila yaliyosababishwa na kadhia hiyo.

Johnson amesema kundi hilo linayoyajumuisha mataifa ya Uingereza, Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Canada, Japan na Italia linapaswa kubeba dhima kubwa ya kumaliza janga la Corona na kuufufua tena uchumi wa ulimwengu.

Kiongozi huyo ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo wa kilele ametumia hotuba yake kupigia upatu suala la kuongeza upatikanaji wa chanjo kwa duniani akisema anatumai viongozi wa G7 watafikia makubaliano ya kuchangia dozi bilioni 1 za Covid-19 kuyaisaidia mataifa masikini.

Kansela Angela Merkel (aliyevalia koti jekundu) akiwa kwenye mazungumzo na viongozi wenzake wa Ulaya pembezoni mwa mkutano wa kilele wa G7.

Mapema kabla ya ufunguzi wa mkutano huo, kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema anaamini yeye na viongozi wenzake wa kundi la la G7 watafikia makubaliano ya manufaa kuhusu chanjo za virusi vya corona na kuenzi umuhimu wa kushirikiana kimataifa.

Merkel amesisitiza kwamba itakuwa ni muhimu kwa kundi la G7 kuonesha kwa vitendo kuwa linajali ustawi wa mataifa mengine linapokuja suala la kumaliza janga la virusi vya corona.

"Ninatumai tutafikia matokeo mazuri sana hapa ili kuonesha kwamba siyo tu tunajijali wenyewe lakini pia wale wasio na uwezo wa kupata chanjo, hususan nchi za Afrika pamoja na kwengineko" amesema Kansela Merkel.

Kansela Merkel ambaye anahudhuria mkutano huo wa G7 unaotarajiwa kuwa mwisho kabla ya hajaondoka madarakani baadae mwaka huu amesema serikali itatoa msaada wa dozi milioni 30 ikiwa ni sehemu ya ahadi ya dozi milioni 100 zitakazotolewa  na Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwaka huu.

Viongozi wa G7 wanaandamwa na shinikizo la kutaka mataifa yao yaliyo na uwezo mkubwa kiuchumi  kutoa msaada zaidi wa chanjo kwa mataifa masikini.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema nchi yake itachangia dozi milioni 100 ahadi sawa na ile iliyotolewa na waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau

Kwa upande wake rais wa Marekani Joe Biden amesema Washingtoninalenga kutoa dozi milioni 500 za chanjo kwa mataifa yasiyo na uwezo.

Viongozi wa mataifa mengine ya kundi hilo pia wanatarajiwa kutoa ahadi za michango ya chanjo.

Hata hivyo wakosoaji tayari wamesema kiwango hicho ni kidogo na mataifa tajiri ni sharti yafunge mkwiji na kuusaidia ulimwengu mzima badala ya kutoa mchango wa chanjo kwa njia ya kudunduliza.

No comments: