ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 1, 2021

NEMC Yaandaa Mafunzo Kwa Maafisa Mazingira Ili Kufuzu Katika Ukaguzi Wa Mazingira

 


 Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC), ya andaa mafunzo kwa Maafisa Mazingira kwa lengo la kukuza uelewa ili kufuzu kuwa wakaguzi wa mazingira ambao mwisho wa mafunzo hayo watapewa vitambulisho kuwa wakaguzi rasmi. Vitambulisho hivyo vitatolewa na Waziri mwenye dhamana ya mazingira nchini. Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Menan Jangu, amesema kuwa, lengo la kufanya mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa NEMC  inaongeza uwezo wa kusimamia mazingira kulingana na Sheria ya Mazingira na kukuza uelewa wa namna ya kusimamia mazingira kwenye jamii yetu.

Ameedelea kusema kuwa kuchaguliwa kuwa Mkaguzi wa Mazingira ni cheo kikubwa hivyo kila mtu ambaye amepata fursa hii ya kujifunza na kuweza  kupewa kitambulisho kama Mkaguzi wa Mazingira ana dhamana kubwa katika kusimamia Uhifadhi wa Mazingira Nchini.

“Mkaguzi wa Mazingira anatakiwa kutumia mbinu rafiki katika kuelimisha au kuelekeza mtu ili aweze kutekeleza maelekezo anayopewa kulingana na sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.  Pale ninaposema  kuwa Mkaguzi wa Mazingira ni cheo kikubwa hii ni kutokana na kifungu cha 182 cha Sheria ya Mazingira ambacho kinampa dhamana Waziri mwenye dhamana ya Mazingira  kuteua Mkaguzi wa Mazingira na tutambue kuwa unapoteuliwa unakuwa mwakilishi wa Waziri katika kusimamia mazingira kwenye jamii inayokuzunguka. Hivyo kila mtu atumie nafasi hii kujifunza na kujua jukumu alilonalo ni kubwa.”

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa Sheria kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) Muhandisi Redempta Samwel, amesema kuwa anaamini baada ya kumaliza mafuzo hayo  kila mtu atakuwa amejifunza vya kutosha na atakuwa mfano mzuri katika jamii katika kutekeleza wajibu wake kikamilifu katika usimamizi wa mazingira.

Mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia  31/5/2021 mpaka 2/6/2021.

No comments: