ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 13, 2021

RAIS SAMIA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA KATIBU MTENDAJI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI (EAC)




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akifurahia zawadi ya Picha ya kuchora aliyopewa na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Dkt. Peter Mathuki mara baada ya mazungumzo yao Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 12 Juni, 2021.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkaribisha Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Dkt. Peter Mathuki mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 12 Juni, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Dkt. Peter Mathuki mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 12 Juni, 2021.


Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Dkt. Peter Mathuki akizungumza na Wanahabari mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 12 Juni, 2021 amekutana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki ambaye anakutana na Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo kwa lengo la kujitambulisha na kupokea maelekezo ya kazi.


Katika mazungumzo hayo Mhe. Rais Samia amempongeza Dkt. Mathuki kwa kushika wadhifa wa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya na amemtaka kutekeleza majukumu yake kwa juhudi na maarifa ili Wananchi wa Jumuiya wanufaike na Jumuiya yao.

Mhe. Rais Samia amesema ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya kuna fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zitasaidia kukuza uchumi na kuendeleza miundombinu na kuongeza mshikamano.

Maeneo mengine ambayo Mhe. Rais Samia amemtaka afanyie kazi ni kuimarisha sekta binafsi ambayo ndio inategemewa katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana na kukuza uchumi pamoja na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika masuala mbalimbali yanayofanywa ndani ya Jumuiya.

Pia, Mhe. Rais Samia amemtaka Dkt. Mathuki kusimamia vizuri mpango wa kukuza viwanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuweka mgawanyo mzuri wa viwanda utakaoepusha kuwa na viwanda vya aina moja.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amegusa zaidi ngazi za uongozi na kuwaacha wananchi wakihangaika na vikwazo mbalimbali hivyo ameitaka sekretariet ya Jumuiya hiyo kufanyia kazi changamoto hiyo ili ushirikiano uonekana hadi katika ngazi ya wananchi.

Kwa upande wake Dkt. Mathuki amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kumpokea na kumpa maelekezo ya maeneo ya kutilia mkazo katika utendaji wake na amemuahidi kuchapa kazi kwa nguvu zake zote ili kutekeleza maelekezo na matarajio ya Waheshimiwa Marais.

Dkt. Mathuki amekiri kuwa juhudi kubwa zinahitaji kuimarisha sekta binafsi, kuwawezesha vijana, kutekeleza miradi ya ushirikiano ikiwemo ujenzi wa miundombinu inayounganisha nchi na nchi na kupigania lugha ya Kiswahili ili itambulike katika mikutano ya Kimataifa.

Dkt. Mathuki ameongoza Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Martin Ngoga, Rais Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki Mhe. Nestory Kayobera na Naibu Katibu Mtendaji Mhandisi Steven Mlote.






No comments: