Na Dotto Mwaibale, Singida
VIJANA Mkoa wa Singida wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha na kuimarisha huduma za umeme nchini.
Vijana hao wameyasema hayo walipofanya ziara ya kuona jinsi Serikali ilivyowekeza kwenye sekta ya umeme kwa upanuzi wa kituo cha kupozea umeme kilichopo Singida katika ziara iliyoandaliwa na Kaimu Afisa Vijana mkoani hapa Frederick Ndahani.
Ziara hiyo ilijumuisha vijana 100 kutoka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida na viongozi wa vikundi vya vijana walionufaika na mkopo wa mapato ya ndani.
Akizungumka na vijana hao katika ziara hiyo Ndahani aliwaeleza vijana hao kuwa Serikali ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejikita zaidi kutatua changamoto zinazowakabili watanzania na kuhakikisha kila Kijiji kinapata umeme wa uhakika kwa bei nafuu.
Alisema Serikali imepunguza gharama za uingizaji wa umeme wa Wakala wa Nishati Vijiji (REA) majumbani hadi kufikia Sh 27,000/= ambayo ni sawa na kuku wawili tuu.
" Hii ni fursa kubwa kwa vijana wa mkoa wetu wa Singida na Tanzania kwa ujumla na kuhakikisha tunaanzisha viwanda vidogo vidogo kwenye maeneo yetu ili umeme huu uweze kutunufaisha na kuongeza pato la Taifa," alisema Ndahani.
Ndahani aliwataka vijana hao kubadilika kifikra wawe na maono ya kujiajiri badala ya kutegemea ajira kutoka Serikalini au makampuni binafsi.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwa vijana kwa kuwapatia mafunzo ,stadi mbalimbali pamoja na mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Aidha Ndahani amewahimiza vijana hao kusoma kwa bidii ili elimu watakayoipata iweze kuwasaidia kubuni miradi itakayo waingizia kipato.
Kwa upande wake Mhandisi wa kituo cha kupozea umeme Elikana Yona alisema kituo hicho kimeongezewa uwezo wa kupooza umeme kutoka KV 200 hadi kufikia KV 400 hivyo kusaidia kuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi ya viwanda na majumbani na kuwatoa wasiwasi vijana hao wa upatikanaji wa umeme nchini.
Vijana hao wamepongeza jitihada za Serikali ya kuendeleza ujenzi wa bwawa la kufua Umeme la Mwalimu Nyerere na kuimarisha sekta hiyo mhimu kwa maendeleo ya nchi.
Vijana hao walitumia nafasi hiyo kumshukuru Ndahani kwa kuratibu ziara hiyo ya mafunzo ya kutembelea miradi inayofanywa na Serikali.
Katika ziara hiyo vijana hao walitembelea mitambo ya zamani ya kupozea umeme na mitambo mipya ya kisasa inayojengwa.
No comments:
Post a Comment