ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 23, 2021

VIONGOZI TOENI MOTISHA KWA WATUMISHI WA UMMA ILI WAONGEZE UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI WAO


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu kufunga rasmi kikao kazi cha mwaka cha viongozi hao kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.

Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) kabla ya Waziri huyo kufunga rasmi kikao kazi cha mwaka cha viongozi hao kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi cheti cha utendaji kazi mzuri kwa mmoja wa wakilishi wa taasisi iliyoshinda, kabla ya Waziri huyo kufunga rasmi kikao kazi cha mwaka cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini kabla ya Waziri huyo kufunga rasmi kikao kazi cha mwaka cha viongozi hao kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


Na. James Mwanamyoto-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu, amewataka Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini kujenga utamaduni wa kuwapatia motisha Watumishi wa Umma ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao kwa lengo la kuwajengea ari ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na Serikali kupitia taasisi zake.

Mhe. Ummy ametoa wito huo wakati akifunga kikao kazi cha mwaka cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.

Mhe. Ummy amefafanua kuwa, kutoa motisha kwa Watumishi wa Umma ni mojawapo ya jitihada za kuboresha utendaji kazi wa Watumishi wa Umma, hivyo ni muhimu kwa viongozi kuzingatia hilo.

“Motisha si lazima iwe fedha au kitu kikubwa, yaweza kuwa ni kutambua juhudi za Mtumishi wa Umma hata kwa kumpatia cheti ili mtumishi huyo aendelee kufanya kazi kwa bidii na ufanisi mkubwa,” Mhe. Ummy amesisitiza.

Amewaasa viongozi hao, kuwapatia motisha watumishi walio chini yao na wale ambao majukumu yao hayatoi fursa ya kusafiri kikazi mara kwa mara, hivyo amewataka kutojiangalia wenyewe.

Aidha, Mhe. Ummy amewataka viongozi hao, kuwa na utamaduni wa kurekebisha mienendo mibaya ya Watumishi wa Umma wanaowasimamia ili watumishi hao waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na ufanisi.

Amesema ni wazi kuwa, binadamu wanatofautiana kitabia na kimaadili na ikumbukwe kuwa, mtumishi anaweza kuwa anakabiliwa na changamoto za kifamilia ambazo zinakwamisha utendaji kazi wake, hivyo ni wajibu wa viongozi kutatua changamoto hizo ili kuwawezesha Watumishi wa Umma kutoa huduma bora kwa wananchi.

Sanjari na hilo, amewataka viongozi hao ambao ni wasimamizi wa rasilimaliwatu kuwa na utaratibu wa kuwasikiliza Watumishi wa Umma ili kujenga mahusiano mazuri mahala pa kazi.

“Ninyi ni wasimamizi wa rasilimaliwatu, licha ya kusimamia kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo, mnapaswa kuzingatia utu kwa kuwasikiliza watumishi ikiwa ni pamoja na kufahamu mapungufu yao ili kuyarekebisha,” Mhe. Ummy amehimiza.

Awali akimkaribisha Mhe. Ummy kuzungumza na viongozi hao, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka viongozi hao wakirejea kwenye maeneo yao ya kazi kubuni mikakati ya namna ya kutoa motisha kwa watumishi wanaowasimamia ili kuwajengea ari ya utendaji kazi.

Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, motisha si lazima iwe fedha, wanaweza kutengeneza vyeti au kuwaandikia barua ikiwa ni sehemu ya kutambua utendaji kazi wa watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa bidii, maarifa, ufanisi na weledi.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kilihudhuriwa na Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu kutoka kwenye Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretariti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, na kaulimbiu ya kikao hicho ilikuwa ni: “Utumishi wa Umma unaozingatia Haki na Wajibu kwa Maendeleo ya Taifa”.

No comments: