ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 2, 2021

Watumishi Wa Ofisi Ya Rais – Utumishi Wapatiwa Mafunzo Ya Namna Bora Ya Kutoa Huduma Kwa Umma

 

Veronica Mwafisi-Dodoma
Watumishi watakaokuwa wakitoa huduma kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call centre Customer Service) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wanashiriki mafunzo ya namna bora ya kutoa huduma kwa umma kupitia kituo hicho kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Akifungua mafunzo hayo Jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI, Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji amesema, kituo hicho kitasaidia wadau kupewa mrejesho wa masuala ya kiutumishi kwa wakati tofauti na ilivyo sasa ambapo wanalazimika kusubiri wajibiwe kwa barua.

Bw. Ngangaji amesema, utoaji wa huduma kupitia kituo hicho utapunguza adha ya wanaohitaji huduma na kuongeza kuwa, utajenga mahusiano mazuri kati ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora kwani utarahisisha upokeaji wa maoni na malalamiko ya kiutumishi yanayowasilishwa na kuyashughulikia kwa wakati.

“Ifahamike kuwa, uanzishwaji wa kituo hicho hauondoi mifumo rasmi ya utoaji huduma na ushughulikiaji wa malalamiko, bali ni moja ya utaratibu wa kisasa wa utoaji huduma kwa njia ya TEHAMA.” Bw. Ngangaji amesisitiza.

Amefafanua kuwa, Kituo hicho kitaunganishwa na Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Malalamiko (e-malalamiko) ambao umesanifiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Mafunzo hayo ya siku tatu yana lengo la kujenga uelewa wa watumishi juu ya namna bora ya kuendesha kituo hicho na kubadilishana uzoefu wa  ushughulikiaji wa malalamiko na maoni ya wadau ambayo yatakayoboresha uendeshaji wa Kituo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji wa Maadili, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika, amemshukuru Bw. Ngangaji kwa maelekezo aliyoyatoa na kuahidi kuwa kituo hicho kitatumika kujenga taswira nzuri ya Ofisi na Serikali kwa ujumla.

No comments: