ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 26, 2021

CPB kukarabati kiwanda cha unga Arusha

BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Cereals and Other Produce Board of Tanzania - CPB), ina mpango wa kutumia Shilingi Billion 2.3 kwenye ukarabati wa kiwanda cha Unga cha Arusha eneo la Unga Limited katika mikakati yake ya kukifanya kinaongeza uzalishaji wa unga wa sembe toka tani 40 mpaka tani 60 kwa siku.

Akiongea katika mahojiano maalumu ya ufafanuzi kufuatia taarifa potofu kadhaa zilizotolewa hivi karibuni katika mitandao ya kijamii, Meneja wa Kiwanda cha Arusha Bw. Hizza amesema tayari mkandarasi wa kufanya ukarabati huo mkubwa ameshapatikana na kazi inatarajiwa kuanza wakati wowote ule.

Bw. Hizza amesema kwamba hatua hiyo ni moja ya mikakati mingi ambayo Bodi hiyo imepanga kutekeleza katika kuwandolea wakulima tatizo la masoko pamoja na bei kadhalika na upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo ikiwa ni msimamizi katika ubora ndani ya biashara ya nafaka

Amesema Bodi hiyo, ambayo ni taasisi ya serikali chini ya wizara ya Kilimo iliyopewa dhamana ya kufanya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko chini ya Sheria ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Na.19 ya Mwaka 2009, tayari imeshaingia mkataba na wakulima wa ngano kwa kusambaza tani 225 za mbegu bora kwa wakulima wa wilaya tano kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara katika mwaka wa fedha wa 2020/2021.

Bw. Hizza ameeleza kwamba mbali ya usambazaji wa mbegu na kuwahakikishia wakulima soko la ngano, pia CPB imetoa maafisa ugani ambao watakuwa na wakulima katika kipindi chote cha ukulima wa zao la ngano ili kutoa elimu na kuhakikisha uandaaji wa mashamba darasa sehemu mbalimbali kwa wakulima wa ngano.

Amesema CPB kwa kushirikiana na kampuni ya kuzalisha na kusambaza mbegu ya Seed Co itatoa elimu na wataalam kwa wakulima kwenye maeneo hayo ili kuwawezesha kupata mavuno mengi na bora, na kwamba Bodi ilikabidhi mbegu za ngano ya chakula, zenye ubora wa hali ya juu kutokana na kuwa na protini ya kutosha.

“Hivyo ngano itakayovunwa itafaa zaidi kwa matumizi ya nyumbani na viwandani, ambako hutumika kutengeneza mikate, keki, chapati na vyakula vingine.

“Vilevile CPB imewahakikishia wakulima wote wa ngano kununua ngano yote baada ya mavuno ili kuwaondolea wakulima wengi tatizo la masoko pamoja na bei”, ameongezea.

Bw. Hizza ameeleza pia kwamba zaidi ya ekali 3,000 za mashamba ya ngano zimelimwa na wakulima 270 wamesajiliwa na Bodi katika kilimo cha mkataba cha ngano ambapo msimu huu CPB inatarajia kupata tani 7,000 za ngano kutoka kwa wakulima kupitia mpango huo.

Bodi hiyo ina viwanda vilivyopo Mwanza, Arusha, Dodoma na Iringa ambavyo vyote vilikuwa chini ya umiliki wa shirika la Taifa la Usagaji (NMC). Kiwanda kilichopo Arusha ambacho kimetajwa kuwa ni mkombozi mkubwa wa wakulima wa kanda ya kaskazini kinasindika unga wa sembe na ngano pamoja na kununua nafaka ambapo wakulima wameweza kupata soko la uhakika la mazao yao.

Wakulima wengi wa kanda ya Kaskazini wameishukuru CPB kwa hatua zake mbalimbali inazochukua katika kuimarisha uzalishaji, ununuzi na kuongeza thamani mazao ya nafaka, wakiitaja kuwa ni mkombozi wao mkubwa katika sekta hio.

Wakiongea kwa nyakati mbalimbali, wakulima hao wamesema tangu CPB ilipoanza kutekeleza majukumu yake, ahueni ya kupata soko ya mazao yao imekuwa kubwa kuliko wakati wowote ule.

“Siku hizi tunalima kwa amani tukijua kwamba mazao yetu yana soko tayari tofauti na zamani ilikuwa kama tunalima kwa kucheza pata potea”, amesema Bw. Amanieli Mwingia, mkulima wa mahindi mkoani Arusha, baada ya kupokea malipo ya mazao aliyoiuzia bodi mwaka huu.

Bw. Mwingia, hata hivyo, ametoa rais kwamba mikakati ya kumkomboa mkulima inayofanywa na Bodi hiyo isiishie kwenye nafaka pekee bali pia kwenye sekta zingine muhimu kama vile ufugaji na uvuvi ambazo amesisitiza zinahitaji msukumo huo ili kuimarisha tija.

Bi. Petronella Mchechu wa Ngarenaro naye amesema hayo, akiongezea kwamba amefarijika kuona CPB inafanya kazi na wakulima na watafiti mbalimbali katika kudumisha ubora wa nafaka na mazao yalinayozalishwa nchini, na kwamba wakulima wangekuwa mbali zaidi kimaendeleo endapo kama hatua hizo zingekuwa zinachukuliwa toka zamani.

 

No comments: