ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 26, 2021

TLS yaingilia kati sakata la Freeman Mbowe

 


Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimeingilia kati sakata la kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kikitaka aachiliwe au afikishwe kwenye mamlaka za kisheria.

Kiongozi huyo wa chama hicho, kikuu cha upinzani nchini, alitiwa mbaroni alfajiri ya kuamkia Julai 21 akiwa hoteli ya Kingdom mtaa wa Ghana alikokifikia kwa ajili ya kushiriki kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Hata hivyo, siku iliyofuata Msemaji wa Polisi nchini, David Misime aliueleza umma kuwa Mbowe anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi na kuua viongozi wa Serikali.

Msimamo wa TLS umetolewa leo  Jumapili  Julai 25, 2021 na rais wa chama hicho, Dk Hoseah  katika tamko lake lililosambazwa kwenye mitandao ya kijamii mbalimbali.

Akinukuu, Katiba ya Tanzania, Dk Hoseah amesema Ibara ya 21(1) inatoa haki ya kujumuika na Ibara ya 13(1) inatoa masharti ya watu wote kuwa sawa mbele ya sheria.  

Dk Hoseah ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), amesema kitendo cha kumkamata usiku wa manane Mbowe na wenzake, kwa sababu ya kuandaa kongamano ni ukiukwaji wa Katiba na sheria za nchi.

Amesema kufanya kongamano haijawahi kuwa kosa la jinai kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi. Amefafanua kuwa ikiwa kuna tuhuma nyingine dhidi yake bado kwa sheria za nchi alipaswa kufikishwa kwenye mamlaka za kisheria  na si kuendelea kuzuiliwa.

“Natoa mwito kwa mamlaka kumwachia huru kwa sababu kuendelea kumshikilia ni kukiuka utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria.

TLS  tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu suala hili na tutatoa msimamo wetu na mwelekeo baada ya mashauriano kufanyika kupitia baraza la uongozi," amesema Dk Hoseah.

No comments: