Timu za Mbweni JKT ya jijini Dar es salaam na TAMISEMI QUEENS kutoka jijini Dodoma zimegeuka kuwa mwiba mkali kwa timu nyingine zinazoshiriki mashindano ya Netiboli ligi daraja la kwanza yanayoendelea katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid ya jijini Arusha baada ya kufanikiwa kuzifunga timu zote ilizokutana nazo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mchezo wa Netiboli Tanzania (CHANETA) Judith Ilunda hadi kufikia jana bingwa mtetezi timu ya JKT Mbweni ndiyo ilikuwa ikiongoza ligi hiyo baada ya kucheza michezo 5 na kushinda michezo yote, na kujikusanyia alama 10, na kufuatiwa na TAMISEMI QUEENS ambayo ilijikusanyia alama 8 baada ya kucheza michezo 4.
Magereza Morogoro inashika nafasi ya 3 kwa kuwa na alama 8 baada ya kucheza michezo 6, huku nafasi ya 4 na ya 5 zikichukuliwa na timu za majeshi za Uhamiaji na Mgulani JKT ambapo Uhamiaji ina alama 6 baada ya kucheza michezo 5 huku Mgulani JKT ikishika nafasi ya 5 baada ya kucheza michezo 5.
Nafasi ya 6 imeshikwa na timu ya Polisi ya Arusha yenye alama 3 baada ya kucheza michezo 6, huku nafasi ya 7, 8 na 9 zikichukuliwa na Ihumwa Dream Team, Eagles na Jiji Arusha.
Ligi hiyo iliendelea tena leo ambapo asubuhi JKT Mbweni ilicheza na Ihumwa Dream Team na matokeo JKT Mbweni ilishinda kwa magoli 78-30, nayo timu ya TAMISEMI QUEENS ilicheza michezo miwili na kufanikiwa kushinda michezo yote.
Katika mchezo wa kwanza, TAMISEMI QUEENS ilicheza dhidi ya JKT Mgulani na kuifunga magoli 46-32 na katika mchezo wa pili TAMISEMI QUEENS ilicheza dhidi ya Uhamiaji na kuifunga magoli 49-32.
Kwa matokeo hayo TAMISEMI QUEENS na JKT Mbweni zote zimecheza michezo 6 kila mmoja, na kufanikiwa kushinda michezo yote, hali inayoashiria upinzani mkali katika kinyang’anyiro cha kumtafuta bingwa wa ligi daraja la kwanza netiboli nchini mwaka huu.
Timu hizo mbili zinatarajiwa kukutana katika mchezo wa mwisho wa kuhitimisha mashindano ya ligi daraja la kwanza utakaofanyika tarehe 29 julai, 2021, mchezo ambao huenda ndiyo utakaoamua hatma ya ubingwa wa netiboli ligi daraja la kwanza mwaka huu.
No comments:
Post a Comment