Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Khamis Juma amesema serikali inathamini michango ya wanasayansi katika uibuaji wa tafiti mbalimbali zenye lengo la kuondoa changamoto zinazokabili taifa.
Alisema hayo jana wakati akizindua mradi wa kuimarisha mifumo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini Tanzania wenye lengo la kwenda sanjari na maendeleo endelevu ya dunia.
Mradi huo unafanyika chini ya ushirikiano wa UNESCO, Tume ya Taifa ya UNESCO, Wizara ya Elimu, Sayansi na teknolojia na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Alisema kutokana na umuhimu wa mradi huo serikali imewataka wadau wote kutoa ushirikiano wa kutosha kuweka misingi ya utafiti, uendelevu wake na kusaidia watunga sera kutambua nguvu kubwa ya taifa katika kusaidia kubadili maisha ya wananchi kupitia tafiti.
Katibu Mkuu huyo akifafanua zaidi alisema kwamba ni matumaini ya serikali washiriki watasaidia kuchangia uandishi wa msingi wa ripoti itakayowezesha uimarishaji wa hatua za kuimarisha sera na ubunifu katika sayansi na teknolojia.
Aliwataka wadau kuunga mkono jitihada za serikali na UNESCO za kuimarisha utafiti wa kisayansi na ubunifu ili kuchangia kiuchumi na kujikinga na majanga
Mkuu wa Ofisi, UNESCO Dar es Salaam, Dos Santos Tirso katika hotuba yake ilyosomwa na Mkuu wa kitengo cha Elimu UNESCO, Bi. Faith Shayo alisema kwamba shirika hilo limefurahishwa kufanyakazi na serikali kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.
Alisema mradi huo umelenga kusaidia Mataifa Wanachama kutekeleza Pendekezo la Watafiti wa Sayansi na Teknolojia 2017, kwa nchi sita za Afrika tangu Septemba 2020 za Ghana & Sierra Leone,Tanzania, Namibia, Zimbambwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mradi utatekelezwa kwa awamu mbili na awamu ya majaribio ya: Septemba 2020 -Agosti 2022 na Awamu ya II: Septemba 2022- Agosti 2025. Bajeti iliyotengwa kwa awamu ya majaribio ya mradi nchini Tanzania ni Dola za Marekani 250,000.
Awali akitambulisha mradi huo Mkuu wa kitengo cha Sayansi asilia na Mratibu wa mradi huo kutoka UNESCO, Bw. Keven Robert alisema kuwa mradi huo utawezesha kusaidia nchi kuimarisha mifumo ya sayansi, teknolojia na utafiti.
Aidha mradi huo pia utasaidia kuimarisha taasisi za kisayansi kufanya tafiti na kuweka mazingira wezeshi ya kufanya tafiti za kisayansi ambazo zitasaidia katika kutatua changamoto za wananchi, kukabiliana na majanga yakiwemo magonjwa mbalimbali na pia kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
Robert alisema kuwa mradi huo utakuwa na maeneo10 ya utekelezaji ambapo baadhi ya maeneo ni pamoja na kuangalia uwekezaji katika tafiti za kisayansi ambapo matokeo ya tafiti hizo zinapouzwa zinaweza kuimarisha uchumi ya nchi.
“Mfano katika kipindi hiki cha janga la Corona yapo mataifa yaliyofanya tafiti za kisayansi na kutengeneza chanjo hivyo zinapouzwa mataifa hayo yamekuwa yakipata fedha na kukua kiuchumi,” alisema Robert.
Alitaja maeneo mengine yatakayoangaliwa katika mradi huo kuwa ni kwa namna gani tafiti za kisanyansi zinasaidia wananchi na kwa namna gani wananchi wanashirikishwa kwenye tafiti kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
No comments:
Post a Comment