ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 29, 2021

Wachimbaji wadogo na malalamiko yasiyo na Mwisho Busega, Simiyu

Samirah Yusuph
Busega. Fukuto la mgogoro wa wachimbaji wadogo katika mgodi wa Imalamate wilayani Busega  Mkoa wa Simiyu baina ya wamiliki wa leseni na wenye mashamba kuhusu mgawanyo wa mazao ya dhahabu linaendelea kuibua malalamiko.

Wachimbaji hao wamekuwa wakidai kuwa hawatendewi haki na wamiliki  wa leseni katika mazao yanayopatikana hali inayowalazimu kutoa mgao hata katika huduma za kijamii kama usimamizi na ulinzi ambazo zilipaswa kulipwa na wenye leseni.

"Licha ya kuwa utaratibu unaelekeza majukumu ya mmliki wa leseni  lakini bado walinzi na "inspectors" tunawapa mgao jambo ambalo linakuwa ni unyonyaji kwa wachimbaji wadogo" alisema Jumanne Tembe mmoja wa wachimbaji wadogo katika mgodi wa Imalamate.

Licha ya malalamiko hayo Baadhi ya wachimbaji wamelaumu wasimamizi wa mgodi kutoza pesa ya usafi na kuweka alama katika mifuko ya mawe bila kutoa risiti jambo ambalo wamelishuku kuwa ni upotevu wa mapato ya serikali pamoja na dhuruma kwa sababu pesa wanayotozwa ni kubwa.

"Mfuko mmoja unalipiwa tsh27,000 unapo utoa kwenye duara na kuufikisha katika uzio ili uwekewe alama lakini pesa inapokelewa bila kutolewa risiti ni bora malipo yafanyike na risiti itolewa ili ijulikane pesa hiyo inaenda wapi na inafanya nini".alisema Amos Mwambebo mchimbaji katika mgodi huo.

Akitoa ufafanuzi dhidi ya mgawanyo wa mazao ya dhahabu yanayopatikana Afisa madini wa mkoa wa Simiyu Amin Msuya alisema kuwa mgawanyo unakakwenda katika makundi manne na kuyabainisha makundi hayo kuwa,

"Mrahaba wa serikali asilimia saba, mmiliki wa shamba asilimia 10, mmiliki wa leseni asilimia 20 na mwenye
 Duara anabakiwa na asilimia 70, mwenye jukumu la kulipa usimamizi na ulinzi ni mmliki wa leseni katika asilimia zake".

Akitatua kero hiyo mkuu wa wilaya ya Busega, Gabriel Zakaria aliwataka wasimamizi wa mgodi kutekeleza maagizo ya serekali ikiwa ni pamoja na kufuata mikataba ya makubaliano ya mgao, kuboresha miundombinu ya barabara na upatikanaji wa huduma za kijamii.

"Mapato ya serikali ni lazima yakusanywe, haki itendeke kwa kila mmoja hakuna sababu ya kuendelea kuwa na mgogoro halikuwa utaratibu upo wazi katika migodi niwakati wa  kutekeleza ili kila mmoja anufaike na madini yaliyopo".

Mwisho.

No comments: