Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na taasisi za fedha imejipanga kuagiza mbegu bora na kuzigawa kwa wamiliki wa viwanda vya mafuta nchini ili waweze kuingia mikataba na wakulima wakubwa, au vyama vya Ushirika ambavyo vitaingia mikataba na wakulima ili kuwapatia mbegu hizo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na tija katika mazao ya kilimo.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 24 Julai 2021 katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma wakati akizindua shughuli za Kampuni ya PASS Leasing ambayo ni kampuni tanzu ya PASS Trust, iliyosajiliwa na benki kuu, kutoa huduma za kukopesha mikopo ya zana za kilimo bila dhamana.
Waziri Mkenda amesema kuwa changamoto inayoikabili sekta ya kilimo ni uchache wa uzalishaji mbegu nchini, Uwezeshaji wa Maafisa Ugani pamoja na Zana za Kilimo, hivyo ili kukabiliana na changamoto hizo tayari serikali imekuja na muarobaini.
Mafuta ya alizeti ni mazuri kuliko mengine hivyo katika kuimarisha afya za watanzania, mkakati huo wa kuongeza uzalishaji na tija katika mazao ya mafuta hususani zao la alizeti itaimarishwa ambapo tayari mikoa mitatu ya Simiyu, Singida na Dodoma imewekwa kama mikoa ya mfano katika uzalishaji.
Akizungumzia kuhusu Maadhimisho hayo, Waziri Mkenda amesema kuwa wiki ya kilimo kwa PASS Trust ambayo inafanyika jijini Dodoma, chini ya kauli mbiu “Pamoja tuwezeshe upatikanaji wa fedha kwa kilimo endelevu, kwa ushirikiano na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe Antony Mtaka imeandaliwa wakati muafaka ambapo serikali inatilia mkazo kampeni zinazolenga kuinua kilimo cha mazao ya kimkakati nchini.
Katika hafla hiyo, Waziri Mkenda amezindua Kampuni ya Pass Leasing ya kukopesha wakulima zana za Kilimo bila dhamana na kwa riba nafuu pamoja na kukabidhi zana za kilimo za kisisa kwa wateja wanne wa kwanza ambazo ni matrekta matatu na mtambo wa kuvunia mpunga.
Waliokabidhiwa ni; Kampuni ya Magic LN Suppliers ya Chalinze mkoani Pwani ambayo imekopeshwa mtambo wa kuvunia mpunga wenye thamani ya sh. Mil. 79, Anthony Maganga wa Igunga Tabora aliyepata Trekta aina ya New Holland lenye thamani ya sh. Mil. 54.
Wengine ni Japhet Ndebezi wa Chamwino mkoani Dodoma aliyekopeshwa Trekta lenye thamani ya sh. Mil. 46 na Mwandishi wa Habari Mwanzo Millinga wa Ruvuma ambaye amepata Trekta aina ya John Deere pamoja na majembe yake lenye thamani ya sh. Mil. 71.4.
Makabidhiano hayo yamefanyika mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka na viongozi wa Taasisi Pass Trust pamoja na wananchi waliohudhuria Wiki ya Pass Trust kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Mikopo inayotolewa na Kampuni ya Pass Leasing kwa upande wa kilimo ni; zana za kuwezesha uzalishaji wa kilimo cha mazao, usindikaji, uhifadhi wa mazao na usafirishaji.
Kwa upande wa uvuvi ni; vifaa uvuvi na mashine zote zitumikazo kuongeza tija katika sekta ya uvuvi. Ufugaji nyuki ni; Vifaa mbalimbali vya kuongeza tija na thamani katika sekta ya nyuki na mazao yatokayo na na nyuki.
Ufugaji ni; Vifaa na mashine za kuongeza tija katika sekta ya ufugaji na kwa upande wa misitu ni vifaa na mashine zitumikazo kwenye misitu na viwanda vya mbao.
No comments:
Post a Comment