ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 26, 2021

Majaliwa: Tumedhamiria Kuboresha Maslahi Ya Watumishi, Chapeni Kazi


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini wakiwemo waalimu, hivyo amewataka wafanye kazi kwa bidii na maarifa.

Mheshimiwa Majaliwa aliyasema hayo jana (Ijumaa, Julai 23, 2021) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika kijiji cha Chinokole na Shule ya Sekondari ya Kassim Majaliwa.

Alisema licha ya kuboresha maslahi ya watumishi pia Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya sekta ya elimu kama ujenzi wa vyumba vya madarasa, maabara, matundu ya vyoo na nyumba za walimu katika shule za msingi na sekondari nchini.

Waziri Mkuu alisema lengo la maboresho hayo ni kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora yatakayowafanya wapende masomo na kuongeza ufaulu. “Pia tunajenga mabweni ili kuwawezesha wanafunzi kukaa shuleni na kupata muda mwingi wa kujisomea.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania waendelee kushikamana na kushirikiana na Serikali yao kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa ajili ya manufaa yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Pia, Waziri Mkuu alikagua miundombinu ya shule ya Sekondari ya Kassim Majaliwa ukiwemo mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu ambapo alisema ameridhishwa na mradi huo na kuwataka waliokabidhiwa jukumu la kusimamia wahakikishe mradi huo unakamilika kwa wakati.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema Serikali imeadhamiria kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike kwa lengo la kumuwezesha kutimiza ndoto zake kielimu. ”Tunataka watoto wa kike wasome bila usumbufu ili waweze kutimiza ndoto zao.”

Katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa, Waziri Mkuu alisema Serikali imeanzisha mradi wa ujenzi wa shule za wasichana kwenye maeneo mbalimbali nchini pamoja na kwenye wilaya ya Ruangwa ili kutoa nafasi nzuri kwa mtoto wa kike kupata fursa ya kusoma vizuri akiwa katika mazingira rafiki yatakayo muepusha na changamoto zinazowafanya washindwe kutimiza malengo yao kielimu.

No comments: