ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 2, 2021

BASHUNGWA - ADA ZA TOZO ZA LESENI ZA MATANGAZO ZAPUNGUA KWA 50%

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa kulia akizungumza katika kikao baina yake na Naibu wake Mhe, Pauline Gekul, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa na Kaimu Mkuu wa kitengo cha Sheria kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Evordy Kyando wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya maboresho ya Rasimu ya Marekebisho ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za Mwaka 2020 pamoja na Kanuni za Maudhui ya Utangazaji katika Redio na Televisheni za Mwaka 2018 yaliyotolewa na wadau mbalimbali hivi karibuni.

Na John Mapepele, WHUSM

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa amesema Serikali inakwenda kuondoa asilimia hamsini ya ada za tozo mbalimbali za leseni kwenye marekebisho ya Kanuni za maudhui ya mtandaoni na maudhui ya utangazaji katika redio na televisheni yaliyofanywa hivi karibuni ili kuzalisha ajira na vipato wananchi.

Mhe. Bashungwa ameyasema haya leo Septemba 1, 2021 jijini Dodoma katika kikao cha kupokea taarifa ya maboresho ya Rasimu ya Marekebisho ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za Mwaka 2020 pamoja na Kanuni za Maudhui ya Utangazaji katika Redio na Televisheni za Mwaka 2018 yaliyotolewa na wadau mbalimbali hivi karibuni.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.Mhe, Pauline Gekul na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.

“ Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kwa dhati kufanya marekebisho ya kanuni hizi kwa kuwashirikisha wadau wake ambapo sasa katika kipindi kifupi kijacho tutashuhudia maboresho yanaleta matumaini na mapinduzi makubwa kwenye sekta na wadau wategemee ongezeko la ajira na kuboreka kwa vipato vyao kwa kiwango kikubwa”. Amesisitiza Mhe. Bashungwa

Ameongeza kuwa ada kwa Leseni za ‘simulcasting’ imeondolewa kabisa ambapo ameeleza kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya kuzingatia maoni ya wadau ya kuiomba Serikali tahfifu ya ada husika ili waweze kumudu kulipa bila faini au kulimbikiza madeni ambapo amesema watoa huduma wanatazamiwa kuongezeka kutokana na viwango vya ada kuwa rafiki.

Akitoa taarifa ya maoni ya maboresho ya kanuni hizo kwa viongozi hao wakuu wa Wizara, Kaimu Mkuu wa kitengo cha Sheria kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Evordy Kyando amesema baadhi ya mambo muhimu katika Marekebisho ya Kanuni za Maudhui ya Utangazaji - Redio na Televisheni ni pamoja na kuongeza ukomo wa vituo vya usikivu kwa leseni za Wilayani kutoka kimoja hadi vitatu (3) katika eneo ambamo redio au televisheni ipo ambapo ameeleza kuwa marekebisho haya yanatazamiwa kuongeza usikivu wa redio na Televisheni katika maeneo yenye milima na mabonde.

Aidha, Kanuni ya 37 ya mwaka 2018 imerekebishwa kwa kufuta kanuni ndogo ya (2) iliyozuia kuungana na kituo kingine ili kutoa matangazo (hookup) bila kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambapo kwa sasa kituo kitatakiwa kinatioa taarifa tu kwa TCRA tofauti na awali.

Pia Kyando amesema marekebisho mengine yamefanywa kwenye Kanuni ya 37(4) kwa Kuondoa masharti ya mgeni kusindikizwa studio kwa lengo la kuondoa kabisa masharti yaliyotaka mgeni wa kituo chochote cha huduma ya maudhui kutoruhusiwa kutembelea kituo hicho mpaka awe ameongozana na Afisa wa Serikali au TCRA

Kwa upande wa Kanuni za maudhui ya Mtandaoni, Kyando ameyataja mambo muhimu yaliyofanyiwa marekebisho katika Kanuni hizi kuwa ni pamoja na kuondoa masharti kwa watoa huduma wa Internet Cafes (Kanuni ya 2 na 13), Kuondoa masharti ya kuwa na leseni kutokaTCRA (Kanuni ya 3), Kuondoa Leseni za ‘Simulcasting’ ambapo mtoa huduma wa maudhui ya mtandaoni kwa simulcasting hatalazimika kukata leseni nyingine wala kulipia ada tofauti anaporusha maudhui yaleyale anayorusha katika redio au televisheni asilia.

Pia, kuondoa wajibu kwa watoa huduma kutunga sera ya matumizi na kufunga vifaa vya kuchuja maudhui mabaya (kanuni ya 9), Kuondoa zuio la ‘Simulcasting’ kwa redio za Wilayani na Mikoani na Kuondoa zuio la Matangazo ya Betting na michezo Mingine ya kubahatisha.

 

No comments: