ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 23, 2021

RAIS SAMIA AMWAGA MABILIONI UJENZI WA OFISI ZA SANAA NA MICHEZO

Katibu Mkuu wa Sanaa, utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akionesha picha ya jengo jipya la Wizara hiyo mara baada ya kusaini Mkataba wa ujenzi wa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Septemba 22,2021 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Sanaa, utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi(kulia) wakikabidhiana Mikataba ya Ujenzi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulid Banyani.
Picha ya pamoja baina ya Katibu Mkuu na Menejimenti ya Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo katika pamoja na viongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

Na John Mapepele- WSUM, Dodoma

Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kujengewa jengo la TZS Bilioni 22.843 makao makuu jijini Dodoma na mkataba wa ujenzi tayari umesainiwa kati ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulid Banyani.

Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini Septemba 22, 2021 jijini Dodoma, Dkt. Abbasi amesema jengo hilo litakuwa na ofisi za kisasa pamoja zenye mahitaji yote yanayohusika katika sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo.

“Hakika hii ni thamani kubwa kwa sekta hizi na jengo hili ni la kwanza kubwa na la thamani zaidi na kali zaidi tangu kuasisiwa kwa sekta hizi kabla na baada ya Uhuru”. Amefafanua Dkt Abbasi

Aidha, Dkt. Abbasi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa jengo hilo ambapo amesema Mhe. Rais amefanya maamuzi magumu na makini katika kuboresha sekta hizi ambazo ni nguvu laini ya nchi.

Ameongeza kuwa tayari serikali imetenga fedha hizo na zitatolewa kulingana na taratibu za Serikali ambapo linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24 sawa na miaka miwili kuanzia sasa.

Amewahimiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambao ni watekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo pamoja Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao ni wasanifu na wabunifu wa majengo hayo kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa kuwa wao ni mabingwa na wameaminiwa kwa uzoefu wao katika masuala ya ujenzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulid Banyani ameishukuru Wizara na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwaamini na kuwapa kazi ya ujenzi wa majengo ya Serikali kwa kuwa waliomba na wamepewa kazi hiyo na kuahidi kuitekeleza kwa ubora na kwa wakati kama ilivyopangwa kulingana na bajeti waliyopewa.

Naye Katibu wa Kuratibu Serikali Kuhamia Dodoma Bw. Meshaki Bandawe amesema Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo inakuwa Wizara ya nane kukamilisha taratibu za utiaji wa Saini Mkataba wa ujenzi ambapo ameipongeza kwa hatua hiyo.

Amefafanua kuwa mpango wa Serikali kuhamia Dodoma umerahisisha wizara kuwa na majengo yao na zipo katika eneo moja hatua inayorahisisha wananchi kupata huduma kwa wakati.

Bw. Bandawe ameongeza kuwa majengo ya Wizara yanayojengwa katika awamu ya pili yapo 24 ambapo hadi sasa Wizara nane ikiwemo ya Sanaa, Utamaduni na Michezo zimekamilisha taratibu za ujenzi huo, hivyo zimetekeleza agizo la Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa Septemba 08, 2021 la Wizara zote zikamilishe taratibu za ujenzi wa awamu ya pili ifikapo Septemba 30, 2021.

No comments: