Advertisements

Wednesday, September 22, 2021

Tundu Lissu Afutiwa Kesi


Kesi ya jinai namba 208/2016 ya Jamhuri dhidi ya Tundu Lissu, Jabir Idrissa na wenzao wawili imefutwa katika Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Septemba 22, 2021.

Kesi hiyo imefutwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) chini ya Kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo ya Makosa ya Jinai, ambapo DPP ameieleza Mahakama kuwa upande wa Jamhuri hauna nia ya kuendelea na shauri hilo, na sasa watuhumiwa wote wako huru.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni jinai ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Washtakiwa hao kwa pamoja walikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Ilidaiwa kwamba, Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’ Katika shtaka la pili walidaiwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob alidaiwa, Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Mehboob pia alidaiwa kuwa alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti. Sasa washtakiwa wote wapo huru. 

No comments: