ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 5, 2021

SERIKALI KUFUNGA RADA SABA ZA HALI YA HEWA NCHINI

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akizungumza katika kikao kazi chake na uongozi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, Dkt. Agnes Kijazi akitoa taarifa ya Mamlaka hiyo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, wakati alipotembelea na kukagua utendaji kazi wa Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa Hali ya Hewa kutoka Mamlaka ya Hewa (TMA), Dkt. Hamza Kabelo, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, namna wanavyosoma taarifa za hali ya hewa katika Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi, akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, wakati alipotembelea na kukagua utendaji kazi wa Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.

Serikali imeingia mkataba kwa ajili ya ujenzi wa rada mbili za mwisho za Hali ya Hewa ili kufikisha mtandao wa rada saba zinazotarajiwa kufungwa katika mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro kwa ajili ya kuboresha ukusanyaji na utoaji wa taarifa za hali ya hewa nchini.

Aidha, Serikali imekwishafunga rada tano za hali ya hewa ambapo kati ya hizo rada tatu zimeshafungwa katika mikoa ya Dar es Salaam (Bangulo), Mwanza (Kiseke) na Mtwara (Mikindani) na tayari zimeshaanza kufanya kazi na rada mbili zitakazofungwa katika mikoa ya Mbeya (Kawetire) na Kigoma (Nyamoli) ziko katika hatua za mwisho za utekelezaji.

Ameyasema hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara akiwa jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambapo pamoja na mambo mengine ameipongeza Mamlaka hiyo kwa ufanisi na utendaji kazi mzuri ndani na nje ya nchi.

“Niwapongeze uongozi na watumishi wa Mamlaka hii kwani utendaji wenu umekidhi mahitaji ya ndani na nje ya nchi na kutunikiwa vyeti vya ubora wa huduma”, amesema Naibu Waziri Waitara.

Naibu Waziri Waitara amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kutobweteka na mazuri yanayoendelea kutekelezwa na Mamlaka hiyo na badala yake kuendeleza kubaini na kufatilia mwenendo wa hali ya hewa, vimbunga baharini, hali mbaya ya hewa, upepo mkali kwa ajili ya sekta za usafiri wa anga, majini, ulinzi, kilimo, uvuvi, utunzaji wa misitu na utalii.

“Taarifa mnazozitoa zinaleta tija kwa sekta zote kwani nimejaribu kufatilia sana hata watu wa meli, anga, kilimo na ujenzi wa miundombinu inayoendelea wanapata taarifa zote na kwa usahihi”, amesisitiza Naibu Waziri Waitara.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo na kuisimamia taasisi hiyo kwa ustawi wa maendeleo ya nchi yetu hasa katika karne ya sasa ambayo masuala ya tabia nchi yamekuwa mtambuka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, amesema kuwa taasisi hiyo imeanzishwa mwaka 2019 chini ya Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 ikiwa na majukumu ya kutoa, kuratibu na kudhibiti huduma za hali ya hewa nchini.

Ameongeza kuwa Mamlaka hiyo ina mitambo ya kisasa pamoja na wataalamu ambao wamesaidia kuboresha sana utabiri kwani kiwango cha utabiri usahihi wake umefikia zaidi ya asilimia 80 hapa nchini.

Naibu Waziri Waitara yuko jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzungumza na uongozi na watumishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake.

No comments: