Na Mwandishi Wetu – Moshi
Ushiriki wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika maonesho yanayofanyika mjini Moshi kuelekea maadhimisho ya siku ya chakula Duniani, yameipa fursa ofisi hiyo kunadi sera zake kwa wananchi zinazowataka kisheria wakulima, kulipa tozo za kilimo cha umwagiliaji.
Akizungumza na baadhi na wananchi waliotembelea banda la taasisi hiyo, Bw. Mohamed Mcheni Afisa Kilimo Mwandamizi amesema kuwa, taratibu zote za ukusanyaji wa ada umekamilika na kutangazwa katika gazeti la serikali, “Kwa mwaka huu wa fedha na miaka inayoendelea tutaendelea kukusanya asilimia tano (5%), na kabla ya kulipa, skimu inatakiwa isajiliwe.” Alisisitiza.
Aidha, Bw. Mcheni alisema kuwa Asilimia tano hiyo ni sawa na wastani wa gunia moja kwa hekari kwa zao la mpunga na aliendelea kufafanua kuwa, chama cha wakulima katika skimu za kilimo cha umwagiliaji zinatakiwa kulipa ada ya usajili kiasi cha shilingi laki moja na elfu sabini na tano (175,000/-) ambapo shilingi laki moja ni ada ya mwaka na shilingi elfu sitini ni ada ya usajili, na shilingi elfu kumi na tano ni ada ya maombi ya usajili.
Alitoa wito kwa wakulima kulipa ada ya asilimia tano (5%) ya wastani wa mavuno kwa msimu wa mwaka kwa hekari.
Maonesho kuelekea maadhimisho ya kilele cha siku ya Chakula Duniani yenye kauli mbiu unayosema inayosema “Zingatia Uzalishaji na Mazingira Endelevu kwa lishe na Maisha Bora” yanafanyika Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro katika kiwanja cha shule ya msingi Mandela.
No comments:
Post a Comment