Mratibu wa chama cha wanasheria wanawake nchini (TAWLA) Mkoa wa Arusha, Happiness Mfinanga akitoa elimu ya wosia kwa baadhi ya wananchi wa Wilaya za Babati, Kiteto, Simanjiro, Hanang’ na Mbulu.
Na Joseph Lyimo
WOSIA ni jambo zuri kwa familia nyingi kuweka utaratibu mzuri wa namna ya mgawanyo wa mali zake pindi akifariki dunia na jamii nyingi zimekuwa zikinufaika pindi maagizo yakiwa yameachwa na muhusika.
Mkazi wa kata ya Terrat, Wilayani Simanjiro, Elias John anasema wosia ni mzuri kwani huwa unaondoa mvurugano kwa baadhi ya watu wenye tamaa za mali za marehemu.
“Mtu anachuma mali na mke wake kwa ajili ya watoto wake lakini siku akifariki watoto na mke wanafukuzwa na ndugu wa marehemu hiyo ni kutokana na kutoandika wosia,” amesema John.
Mkazi wa kata ya Orkesumet, Esupat Edward anasema hivi karibuni kulitokea msiba wa dereva wa bodaboda aliyefariki na kuacha mke na watoto wawili, nyumba na pikipiki na ndugu wa marehemu wakataka wamfukuze.
Edward anasema kutokana na wosia uliokuwa umeachwa na dereva huyo wa bodaboda, ndugu wa marehemu walishindwa kumnyang’anya mjane aliyebaki na watoto wake kwenye nyumba na mali zake.
“Ndugu walitaka dereva wa bodaboda akazikwe makaburini lakini madereva wenzake wakashinikiza azikwe pembeni ya nyumba yake na ndugu walipokataa madereva hao wakamzika kwa nguvu na hadi sasa kaburi lipo nje ya nyumba huku mjane na watoto wakimiliki mali za marehemu,” amesema.
Kiongozi wa kimila wa jamii ya wafugaji, Laigwanani Michael Saibul amesema suala la kuandika wosia ni jambo zuri kwani linawezesha mtu kuweka mambo yake sawa kwa mustakabali ya mali zake baada ya yeye kuondoka duniani.
Saibul amesema siyo vibaya kwa mtu kuandika wosia wake ili hata kesho asipokuwepo waliobaki wana uwezo wakugawa mali zake kwa utaratibu kupitia wosia aliouandika.
“Bado kuna changamoto kubwa kwa jamii yetu kuona kuwa wosia ni kujiombea uchoro ila ni utaratibu mzuri kwani hata usipoandika wosia utafariki dunia tuu,” amesema Saibul.
Mchungaji wa kanisa la TAG Mjini Babati, John Manimo amesema utaratibu wa kuacha wosia kwa jamii ni mzuri kwani endapo kukitokea msiba hakutakuwa na ugomvi kwani watu watafuata wosia ulivyoandikwa.
“Wosia ni mzuri kwa jamii na endapo kila mtu atakuwa ameacha wosia inakuwa vizuri kwa watu waliobaki wanasoma kilichoandikwa na hakutakuwa na mgogoroa,” amesema Manimo.
Mratibu wa chama cha wanasheria wanawake nchini (TAWLA) Mkoa wa Arusha, Happiness Mfinanga anasema wosia ni kauli au tamko la mdomo au la maandishi linalotolewa kwa hiyari yake akiwa hai juu ya namna mali yake igawanywe mara baada ya kufariki.
Mfinanga anasema mtu ana uwezo wa kuacha wosia wake kwa kuandika au kutamka na zikakubalika kisheria na kutekelezwa pindi mtu akishafariki dunia.
Amesema faida ya kuacha wosia ni kumpa nafasi mtu kuweka mgawanyo wa mali zake pindi akifariki dunia, namna anavyotaka kuzikwa, inampa fursa ya kuchagua nani awe msimamizi wa mirathi pindi akifariki dunia.
“Wosia unaepusha ugomvi na kusababisha amani kwa warithi pindi kukitokea msiba na kisheria mtu anapaswa kuandika wosia akishafikisha umri wa miaka 18,” amesema Mfinanga.
Anasema wosia ni chombo halali cha kuelekeza namna ya kugawanywa mali kwa muhusika kwa warithi wake halali ambao amewachagua na yeye kuagizwa wapatiwe alichoamua.
Anasema endapo mtu akifariki bila kuweka utaratibu mzuri wa kutamka au kuandika wosia, mali yake itabidi igawanywe kwa mujibu wa sheria za nchi.
No comments:
Post a Comment