ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 2, 2021

KATIBU MKUU WIZARA YA MADINI PROF. SIMON MSANJILA ATEMBELEA BANDA LA TANZANIA EXPO 2020 DUBAI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila (katikati) akitembelea mabanda mbalimbali ya Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Tanzania Expo 2020 yanayoendelea Dubai tarehe 1 Novemba, 2021

Mkurugenzi wa Banda la Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai Bi. Getrude Ng’weshemi kutoka TanTrade amempokea Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila ambaye ametembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya Kimataifa ya Expo 2020 Dubai. Katika ziara hii Prof. Msanjila aliambatana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwase, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini Bw. Augustine Ollal, na Kaimu Meneja wa Uwekezaji na Mipango kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Bi. Nsalu Nzowa.

Dhumuni la ziara hii ilikuwa ni kujionea na kutahmini hali halisi ya maonesho ya Expo 2020 Dubai ili kuweka mkakati bora zaidi ya ushiriki wenye tija wa Sekta ya Madini na namna bora zaidi ya kuendelea kuzitangaza fursa katika sekta hii kote ulimwenguni kupitia maonesho ya Expo 2020 Dubai.

Katika kutekeleza mikakati hiyo Prof Msanjila aliangalia namna Sekta ya Madini Tanzania inavyoweza kushirikiana na nchi nyingine zinazofanya biashara ya madini ili kufikia masoko mengi makubwa zaidi na ya uhakika, na pia uwezekano wa kupata nafasi ya kukutana ana kwa ana na wadau wa uwekezaji.

Ziara hii ni mwanzo mzuri wa maandalizi ya ushiriki rasmi wa Sekta ya Madini katika maonesho ya Expo 2020 Dubai ambapo kutakuwa na program ya Wiki ya Madini inayoandaliwa na TanTrade ambao ni waratibu maonesho haya kwa kushirikiana na Wizara ya Madini na Taasisi zake. Programu hiyo inatarajiwa kuanza tarehe 23 Februari, 2022 hadi tarehe 03 Machi, 2022.

Prof. Simon Msanjila alitumia nafasi hii kutembelea baadhi ya mabanda ya nchi mbalimbali zinazoshiriki kwenye maonesho haya ya Expo 2020 Dubai akianza na mabanda ya Umoja wa Falmeza Kiarabu – Mobility, India na Senegal. Lengo la kutembelea mabanda haya ni kujionea fursa ambazo nchi hizo zimeleta katika maonesho haya. Maonesho haya yanatoa fursa ya kipekee kwa nchi mbalimbali za Afrika kujifunza, kupata uzoefu, kujitangaza kupitia sekta mbalimbali.

Aidha Mkurugenzi wa banda la Tanzania Bi. Getrude Ng’weshemi ameendelea kusisitiza kuwa ushiriki wa sekta nyingine zinazochochea maendeleo ya kiuchumi ikiwemo Sekta ya Madini ni wa muhimu sana katika kuhakikisha kuwa miradi mikubwa na fursa adhimu na zinazohitaji wawekezaji zinapata nafasi ya kujitangaza kupitia ushiriki huu. Ushiriki huu wa pamoja kama taifa utaibua fursa mbalimbali ulimwenguni za uwekezaji na maendeleo endelevu baina ya Tanzania, nchi nyingine za Afrika na Mataifa mbalimbali ulimwenguni.

No comments: