Advertisements

Thursday, November 25, 2021

SERIKALI YAONDOA VIKWAZO KWA WANAFUNZI WANAOPATA MIMBA WAKIWA SHULENI ILI KUENDELEA NA MASOMO

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 24,2021 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Sekta ya Elimu,Sayansi na Teknolojia katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati akiwasilisha mafanikio ya Sekta ya Elimu,Sayansi na Teknolojia katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 24,2021 jijini Dodoma wakati akizungumzia mafanikio ya Sekta ya Elimu,Sayansi na Teknolojia katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.

Na.Alex Sonna,Dodoma

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako,ameeleza mafanikio ya wizara yake yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara huku akisema Serikali itaendelea kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa fursa za elimu ikiwa ni pamoja na kuruhusu wasichana waliopata ujauzito wakiwa shule za msingi na sekondari kuendelea na masomo yao katika mfumo rasmi.

Hayo ameyaeleza leo Novemba 24,2021 wakati akizungumzia mafanikio ya Sekta ya Elimu,Sayansi na Teknolojia katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.

Waziri Ndalichako amesema wanafunzi waliokatiza masomo yao kwasababu mbalimbali watapewa fursa ya kurejea shuleni.

“Serikali imeamua wanafunzi waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali watapewa fursa ya kurejea shuleni itajumlisha wasichana wanaopata ujauzito wakiwa katika shule za msingi na sekondari ,Wanafunzi hao wataruhusiwa kuendelea na masomo yao katika mfumo rasmi wa Seriaklli mara baada ya kujifungua,”amesema.

WALIOFELI,WADANGANYIFU,WAPEWA FURSA

Pia amesema wanafunzi waofeli,kufanya udanganyifu au utovu wa nidhamu watapewa fursa ya kurudia mitihani na watapewa fursa ya kujiunga na shule za sekondari.

“Utaratibu ulivyo sasa mwanafunzi anapofutiwa mtihani wake wa darasa la saba au ambao watafaulu kufeli mtihani wa darasa la saba au anapokuwa amepata tatizo lolote wakati wa mtihani wa darasa la saba atakuwa hana fursa nyingine,sasa tumeamua wanafunzi waofeli,kufanya udanganyifu au utovu wa nidhamu watapewa fursa ya kurudia mitihani na watapewa fursa ya kujiunga na shule za sekondari,”amesema.

ACHUKIZWA NA UTITIRI WA MICHANGO

Aidha,Prof Ndalichako amezitaka shule ambazo zinawachangisha wanafunzi fedha za michango kuachana na utaratibu huo kwa sababu msimamo wa Serikali ni kutoa elimubilamalipo.

“Na zaidi Dar es salaam nimeambiwa kwamba michango imezidi Ilala Kinondoni achene kuchukua hela za wanafunzi wafundisheni wapate elimu na sio kuwabebesha utitiri wa michango jambo hili halikubaliki,”amesema.

MWELEKEO WA WIZARA NI KUTOA ELIMU BORA


Aidha,Waziri Ndalichako amesema Mwelekeo wa Sekta ya Elimu baada ya Miaka 60 ya Uhuru wa nchi ni kuendelea kutoa elimu bora itakayoipatia jamii maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

UBORESHAJI WA MITAALA

Amesema Serikali itahakikisha kwamba inaboresha mitaala ya elimu katika ngazi zote na kuweka msisitizo zaidi katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Sayansi, Ujasiliamali, Stadi za kazi na masuala mtambuka.

Waziri Ndalichako amesema fani za kimkakati kama vile uhandisi, kilimo, udaktari zitendelea kupewa kipaumbele.

Amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule ili kuendelea kutoa fursa zaidi kwa watoto wa kike na wa kiume.

“Kazi hii inafanyika kwa kasi zaidi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo sambamba na ujenzi wa madarasa 15,000 unaoendelea nchini Serikali inatarajia kujenga shule 1,000 za sekondari za kutwa na shule za sekondari 26 za wasichana katika kipindi cha miaka mitano ijayo,”amesema.

Prof.Ndalichako amesema utekelezaji umeanza kwa shule 274 za kutwa na shule 10 za Wasichana ambapo serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 1,405 mnamo tarehe Novemba, 2021.

ELIMU YA UFUNDI

Amesema elimu ya Ufundi na mafunzo ya ufundi stati itaendelea kuimarishwa ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya ufundi stadi katika Wiaya 29 na Mikoa.

Amesema lengo ni kutoa fursa zaidi kwa vijana kupata ujuzi na umahiri utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

“Kwa msingi huo,mafunzo kwa vitendo yatapewa uzito stahiki sambamba na kuimarisha ushirikiano na viwanda ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira;,”amesema

ELIMU MAALUM

Prof Ndalichako amesema Serikali itaendelea kuimarisha elimu maalum kwa kuhakikisha miundombinu inayojengwa ni rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Aidha, Serikali itaendelea kununua vifaa visaidizi ili kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kujifunza kwa ufanisi zaidi.

Amesema Serikali itaendelea kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa fursa za elimu ambapo wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa sababu mbalimbali watapewa fursa ya kurejea shuleni. Fursa hizo zitajumuisha wasichana ambao wanapata ujauzito wakiwa katika shule za msingi au sekondari.

Pia amesema Serikali itaendelea kutoa elimu bila malipo ili kuhakikisha kuwa watoto wote wakitanzania wanapata elimu bila vikwazo.

Aidha, Serikali itaendelea kutoa mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu katika mwaka wa fedha 2021/2022 bajeti iliyoongezeka kutoka bilion 464 hadi 570

No comments: