Na Mwandishi wetu,Mwanza,
“Uhai wa mtu mmoja ni muhimu kuliko uwepo wa mgodi, uhai wa mtu unathamani kubwa kuliko mgodi wenyewe, uchimbaji salama inapaswa kuwa ajenda katika shughuli zote za uchimbaji madini nchini,”.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko alipotembelea mgodi wa Mhalo uliopo wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza mara baada ya kupata taarifa ya ajali iliyowapata wachimbaji 9 ambapo nane miongoni mwao waliokolewa na mmoja bado hajapatikana.
Akizungumza katika tukio hilo Waziri Biteko ametoa pole kwa waathirika wote waliokuwa kwenye ajali hiyo na kuwataka waokoaji kuendelea na jitihada za kumtafuta Immanuel Isaac mwenye umri wa miaka 26 ambaye mpaka sasa hajapatikana.
Aidha, Waziri Biteko amewataka wachimbaji wote nchini kuhakikisha wanachimba kwa utaratibu na kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa migodi wanaoshughulika na masuala ya ukaguzi na usalama katika maeneo ya migodi.
“Naomba nichukue fursa hii kuwaelekeza wachimbaji wote nchini kuhakikisha mnazingatia usalama mahala pa kazi ili kuepusha matukio ya ajali kama hili lililotokea katika mgodi huu wa Nyamikoma uliopo hapa kijijini Mhalo,” amesema Waziri Biteko.
Katika hatua nyingine, Waziri Biteko amewataka wachimbaji wa madini katika eneo lenye mlipuko wa madini lililogunduliwa na wachimbaji wadogo mnamo tarehe 6 Novemba, 2021 kuhakikisha wanachimba kwa kufuta taratibu na kuzingatia usalama katika shughuli zao.
Pia, Waziri Biteko ameitaka Tume ya Madini pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Ernest Maganga kuhakikisha wanatoa leseni ndani ya wiki mbili katika mgodi huo wa Kiwili uliopo katika kijiji cha Mhalo wilayani Kwimba.
“Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan anatamani wachimbaji wote wa madini nchini watajirike, ongezeni juhudi na maarifa katika utendaji kazi wenu na msiruhusu majungu kati yenu, pendaneni na msiruhusu mtu aje awagombanishe,” amesema Waziri Biteko.
Akijibu ombi la Mbunge wa Jimbo la Kwimba Shanif Mansoor, Waziri Biteko amesema Wizara yake itaangalia uwezekano wa kufungua Kituo cha ununuzi wa madini katika eneo hilo na kumpeleka Afisa Madini atakaye simamia eneo hilo ili Halmashauri ya wilaya ya Kwimba iweze kunufaika na uwepo wa madini katika eneo lao ambapo kwa sasa madini yanasafirshwa kupelekwa Soko la Mkoa wa Mwanza.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Biteko amewasisiza wachimbaji wote katika kijiji cha Mhalo kuhakikisha wanajitokeza kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwaka 2022 iliserikali ijue idadi ya wachimbaji wa madini nchini na kuwataka wachimbaji wote nchini kuhakikisha wanachanjwa ili kuepuka ugonjwa wa uviko-19.
Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Ernest Maganga amesema baada ya tukio la kuanguka kwa nguzo iliyokuwa inashikilia ukuta chini ya shimo katika mgodi wa Nyamikoma, Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Mwanza walifika eneo la tukio na kufanya ukaguzi ambapo watu 9 walikuwa wanaendele na shughuli za uzalishaji ambapo watu 8 walifanikiwa kutoka na mtu mmoja hakuonekana ambapo mpaka sasa juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Pia, Maganga amesema Novemba 6, 2021 wachimbaji wadogo wa madini waligundua uwepo wa madini katika eneo la Kiwili katika kijiji cha Mhalo ambapo Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Mwanza ilifika katika eneo hilo na kuwatambua waliogundua na kuwashauri juu ya uchimbaji salama.
No comments:
Post a Comment