Advertisements

Thursday, May 25, 2023

JKT YAWATAKA WAHITIMU KIDATO CHA SITA 2023 KURIPOTI MAKAMBINI KUHUDHURIA MAFUNZO KWA MUJIBU WA SHERIA


Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.

Jeshi la kujenga Taifa JKT limewataka wahitimu wa kidato cha sita waliohitimu elimu ya Sekondari kwa mwaka 2023 kutoka shule zote za Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria kwa mwaka 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya JKT Chamwino Dodoma Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema vijana hao wanatakiwa kuanza kuripoti katika makambi waliyopangiwa kuanzia June 1 hadi June 11, 2023.

“Sanjari na wito huu JKT limewapangia makambi watakayokwenda kupatiwa mafunzo na wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia tarehe 01 june hadi 11 June, 2023” amesema.

Ametaja makambi wanayotakiwa kuripoti kuwa ni JKT Rwamkoma Mara, JKT Msange Tabora, JKT Ruvu Pwani, JKT Mpwapwa na Makutopora Dodoma, JKT Mafinga Iringa, JKT Mlale Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba Tanga, JKT Makuyuni Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila Kigoma.

Makambi mengine ni JKT Itaka Songwe, JKT Luwa na JKT Milundikwa Rukwa, JKT Nachingwea Lindi, JKT Kibiti Pwani na JKT Oljoro Arusha na kuongeza kuwa kwa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho waripoti katika kambi ya JKT Ruvu iliyopo Mlandizi Pwani ambayo ina miondombinu ya kuwahudumia watu hao.

Ameongeza kuwa “ Orodha kamili ya majina ya vijana hao Makambi ya JKT waliyopangiwa na maeneo ya makambi yalipo na vifaa wanavyotakiwa kuripoti navyo inapatikana katika tuvuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz

Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele anawakaribisha vijana wote waliohitimu kidato cha sita mwaka 2023 kuungana na vijana wenzao ili kujengewa uzalendo, umoja wa kitaifa, kufundishwa stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa” amesema.

Katika hatua nyingine amesema kwa wahitimu watakaokuwa wanajiunga na vyuo zoezi la udahili litafanyika katika makambi wanakopata mafunzo na kutakiwa kuripoti katika makambi wakiwa na nyaraka mbalimbali zitakazokuwa zinahitajika wakati wa udahili ikiwa ni vyeti vya kitaaluma na nyaraka mbalimbali.

No comments: