Advertisements

Monday, May 29, 2023

MCHENGERWA -WANANCHI WA VIJIJI VYENYE MIGOGORO YA MIPAKA HIFADHI YA SERENGETI WAYAJENGA, WAIPONGEZA SERIKALI, WATAKA USHIRIKISHWAJI.

 


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa  amekutana  na kufanya   vikao  na wananchi wa vijiji vyenye  migogoro ya mipaka na Hifadhi ya Serengeti na kuutaka uongozi wa Hifadhi ya Taifa (TANAPA) kuimarisha program za ujirani mwema na  kuwashirikisha wananchi wanaozunguka hifadhi wakati wa kupanga mipango yao ili wananchi  waweze kushiriki kikamilifu kwenye uhifadhi wa raslimali hizo na  kupunguza  migogoro isiyo  ya lazima.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo Mei 28, 2023 wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tarime na kufanya mikutano kwenye vijiji vyote vinavyozunguka  Hifadhi ya Serengeti vilivyokuwa na migogoro na mipaka katika zoezi la uwekaji wa  vigingi vya  mipaka ambapo  wananchi  wa maeneo  hao wamepongeza  kwa hatua hiyo ya Serikali ya kuja na kuwasikiliza na kuahidi kushirikiana na Serikali kwenye uhifadhi.

Mhe. Mchengerwa aliambatana Naibu Katibu Mkuu wa Wizara yake Anderson Mutatembwa na Kamishna wa TANAPA, Afande William Mwakilema na kupokewa na uongozi wa Mkoa wa Mara, uongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime na Mbunge wa Tarime vijijini Mhe. Mwita Waitara ambapo katika mikutano hiyo yote Mhe. Mchengerwa aliongoza vikao hivyo kwa  kuwapa  wasaa wa wananchi kutoa  maoni na mawazo yao na mwisho alitolea ufafanuzi wa hoja hizo na nyingine  kuzichukua kwa hatua zaidi.


Wananchi wamepongeza hatua hiyo ya Waziri Mchengerwa  kwenda na kuwasikiliza  huku wakieleza kuwa kumekuwa  na ushirikishwaji mdogo na  kuiomba Serikali  kupanga  kwa  pamoja ili kuondoa  migogoro isiyo ya lazima.

Diwani wa kata ya Nyanungu Tiboche Richard amesema  kuwa wananchi wa Kata yake wapo tayari kushirikiana na Serikali kwenye  kila jambo endapo  watashirikishwa   na hifadhi.

“Mhe. Waziri napenda kukuhakikishia kuwa leo unatufanya tulale usingizi maana umetumwa na Mhe. Rais wetu kuja kutujengea mahusiano mazuri, na sisi hiki  ndicho  tulichokuwa tunakikosa.” Amesisitiza diwani Richard

Akiwa kwenye mkutano katika Kijiji cha Karakatonga wilayani Tarime, Mhe. Mchengerwa ameutaka uongozi wa TANAPA  kushuka  chini kwa wananchi na kwenda kuzungumza nao kwa kuwa  hifadhi hizo ni za wananchi na wananchi ndiyo wahifadhi namba moja.

Aidha, amesema wazo la uhifadhi wa raslimali   katika taifa  la Tanzania limeasisiwa  miaka mingi ambapo uongozi katika awamu zote toka enzi za baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hadi  Rais Samia Suluhu Hassan  limezingatiwa kwa faida   ya kizazi cha sasa  na baadaye.

Akiwa kwenye Kijiji cha Kegonga, Mhe. Mchengerwa ametoa wito  kwa wananchi  hao kushirikiana na uongozi wa Serikali  wakati wote  na kuacha tabia za kugomea  kwa kuwa kwa kufanya  hivyo wanachochea  migogoro.

“Kwa hiyo wanapokuja  viongozi wa Serikali kuja  kujadili mpango wa matumizi bora ya ardhi wasikilizeni msikatae kusikiliza, shaurini tufanye nini.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Amewataka kutambua kuwa  wahifadhi  ni sehemu ya  jamii yao kwa kuwa baadhi ya watumishi hao ni sehemu ya familia zao na watoto wao.

No comments: