NA MWASHAMBA JUMA
MWENYEKITI wa Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation’ (ZMBF), Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi ametoa wito kwa jamii kuzingatia suala la Usalama wa Chakula ili kujikinga na maradhi yatokanayo na chakula kisicho salama.
Mama Mariam Mwinyi aliyasema hayo, kwenye maadhimisho ya siku ya kimtaifa ya Usalama wa chakuka yaliyofanyika, viwanja vya Mwembekisonge, Wilaya ya Mjini.
Alisema kumekua na ongezeko la maradhi yanayosabishwa na usalama mdogo wa chakula, jambo alilolieleza kuathiri afya kwenye jamii.
Aliiasa jamii, kula vyakula vilivyo salama kwa kufuata mtindo mzuri wa kula pamoja na kufanya mazoezi ili kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa matibabu.
Mwenyekiti huyo wa (ZMBF) alieleza moja ya lengo la kuanzishwa kwa taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” ni kuona namna bora ya kuunga mkono jitihada za Kitaifa na Kimataifa kwenye suala zima la kuimarisha lishe, afya na ustawi wa Wazanzibari ili kukuza maendeleo ya kiuchumi hususan kwa wanawake, watoto na vijana.
Alisema siku ya Usalama wa Chakula duniani ni jambo jema linaloleta uwelewa mpana juu ya mambo yanayohusu usafi na usalama wa chakula katika kupunguza maradhi na kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Hivyo, aliwasihi watunga sera, Mamlaka ya Usalama wa Chakula, wanasayansi, wakulima, wauzaji wa chakula, wapishi, walimu, wanafunzi na watumiaji mbalimbali, kuongeza bidii za pamoja ili kuhakikisha mwamko wa Usalama wa Chakula unaongezeka, Zanzibar.
Pia, Mama Mariam aliwataka watunga Sera na waratibu kuhakikisha wanazingatia sera za udhibiti wa mifumo kwa usalama wa chakula na kuimarisha ushirikiano wao kwa wadau wote na kuhakikisha wanaifahamu miongozo na kuitumia mifumo iliopo katika juhudi za kumlinda mlaji.
Aidha, aliwaasa wafanyabiashara za chakula kwamba wana jukumu la kufuata maelekezo ya viwango vilivyotolewa na mamlaka na kuwaeleza kuwa jukumu la kumlinda mlaji limo mikononi mwao.
Aliisisitiza jamii suala la Usalama wa Chakula ni pamoja na kuzingatia kula mlo uliotimia ili kupata lishe bora zaidi kwa watoto, wazee na wajawazito kwa kuimarisha mfumo wa kinga ulio imara na makuzi mazuri kwa watoto.
“Tujitahidi kula chakula kilicho safi kwa kuzingatia virutubisho na wingi unaofaa au unaohitajika”. Alisisitiza Mama Mariam
Wakati huo huo, Mama Mariam Mwinyi, aliupongeza uongozi wa Wizara ya Afya na wa Wakala wa Chakula na Dawa kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kwa kudhibiti vyakula vinavyoingia na vile vinavyozalishwa nchini kwa kuhakikisha kuwa salama kwa matumizi ya binaadamu.
“Kwa hakika, ukaguzi mnaoufanya kwenye maeneo yanayouzwa vyakula na kuwepo kwa Maabara za kisasa za ZFDA hufanya tujiamini juu ya bidhaa za vyakula zilizopo kwenye soko la Zanzibar kuwa ni salama kwa matumizi ya binaadamu”. Alisifu Mama Mariam.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazurui alisema, Wizara kupitia taasisi zake wanaweka taratibu bora za kudhibiti vyakula vibovu visiingie nchini.
“Tuhakikishe tunakula vyakula bora, usafi wa mazingira na uzalishaji wake, kwa bidhaa zote za mashambani na kwenye mifugo” Alisisitiza Waziri Mazurui.
Pia, aliitaka jamii, kufuata taratibu za kuvuna mara baada ya umwagiliaji na kupigwa dawa kwa mazao na Wanyama.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji kutoka Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDA) Dk. Burhan Othman Simai alisema, jukumu kubwa la taasisi hiyo ni kulinda afya ya jamii katika kuhakikisha bidhaa za chakula, dawa, vipondozi, vifaa tiba na vitendanishi vina ubora, usalama na ufanisi unaotakiwa kwa mujibu wa viwango vya kitaifa na kimataifa.
ZFDA ilianzishwa mwaka 2006 na kufanyakazi rasimi mwaka 2007 kwa mujibu wa Sheria ya Chakula Dawa na Vipodozi Sheria no 2/2006 na marekebisho yake, sheria no 3/2007.
Maadhimisho ya siku ya kimtaifa ya Usalama wa chakuka yenye kauli mbiu, “Usalama wa chakula ni jukumu la kila mmoja wetu”awali yaliambatana na mtembezi ya kilomita tano yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa “Zanzibar Maisha Bora Foundation”, Mama Mariam Mwinyi, kutoka soko la mbogamboga Mombasa hadi viwanja vya Mwembe kisonge.
No comments:
Post a Comment