Na Walter Mguluchuma, Katavi.
Watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kumteka mtoto mdogo wa kike (9) mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya Msingi Mizengo Pinda katika Manispaa ya Mpanda na kisha kumfungia ndani ya chumba kwa zaidi ya siku moja na kutishia kumuua kwa madai vinginevyo walipwe Milioni 50 ili wamwachie.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani amewataja watuhumiwa hao walikamatwa kuhusika na tukio hilo kuwa ni Joseph John(24) Yusuph Sadick (27) wakazi wa Mtaa wa Milupwa , Abraham Kassim(28) Mkazi wa Mtaa wa Misunkumilo Manispaa ya Mpanda na Samwel Nzobe (41) Mkazi wa Mtaa wa Kotasi Manispaa ya Mpanda .
Amesema watuhumiwa hao wote wanne wamekamatwa kufuatia msako mkali uliofanywa na jeshi la Polisi usiku na mchana kufuatilia jeshi hilo la polisi kuwa limepata taarifa ya kutekwa kwa mtoto huyo mdogo wa kike.
Kaimu Kamanda wa Polisi Ngonyani amebainisha kuwa tukio hilo la kikatili la kumteka mtoto huyo lilitokea hapo June 13 majira ya saa nane mchana katika Manispaa ya Mpanda wakati mtoto huyo alipokuwa akitokea shuleni kwenye shule anayosoma ya Mizengo Pinda alikuwa amekwenda kufanya usafi shule.
Ameeleza kuwa wakati akiwa njiani maeneo ya jirani na Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda anaelekea nyumbani kwao ndipo watuhumiwa hao wanne walipomteka mtoto huyo na kumpeleka kusikojulikana na kumtishia kumuua lasivyo walipwe na mzazi wake kiasi cha shilingi milioni 50 ndipo waweze kumwachia akiwa hai .
Baada ya taarifa hizo kuwa zimepokelewa Jeshi la Polisi lilianza mara moja kufanya msako mkali wa kuwasaka wahusika wa tukio hilo msako ambao ulifanyika usiku na mchana katika maeneo yote ya Mkoa wa Katavi ili kuwahakikisha mtoto huyo anapatikana akiwa salama .
Ngonyani amesema ndipo mnamo tarehe 14 June jeshi la polisi lilifanikiwa kumpata mtoto huyo akiwa salama huko katika maeneo ya Mtaa wa Milupwa Manispaa ya Mpanda akiwa amefichwa ndani ndani ya chumba cha mtuhumiwa Joseph John.
Amesema watuhumiwa wote wanaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi juu ya tukio hili na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment