ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 21, 2023

ZANZIBAR KUANZISHA KITUO CHA UTATUZI WA MIGOGORO NJE YA MAHAKAMA


Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar Shaaban Ramadhan Abdalla akifungua Mkutano wa kupokea maoni kuhusu Rasimu ya uanzishwaji wa Kituo hicho cha Utatuzi wa Migogoro nje ya Mahkama (ADR Center) katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi hiyo Mazizini uliohudhuriwa na Wataalam wa Sheria kutoka katika Taasisi za Serikali na binafsi nchini.
Mshauri elekezi Dkt. Fauz Twaib ambaaye ni Jaji Mstaafu na Rais wa Jumuiya ya Wanasheria Afrika Mashariki akizungumza na Wanahabari mara baada ya kukamilika kwa mkutano wa kupokea maoni ya Rasimu ya kuanzisha Kituo cha kutatua Migogoro nje ya Mahkama huko Mazizini Zanzibar.
Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar Shaaban Ramadhan Abdalla (kati kati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mkutano wa kupokea maoni kuhusu Rasimu ya uanzishwaji wa Kituo hicho cha Utatuzi wa Migogoro nje ya Mahkama (ADR Center) uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi hiyo Mazizini na kuhudhuriwa na Wataalam wa Sheria kutoka katika Taasisi za Serikali na binafsi nchini. Picha na Faki Mjaka.

Serikali kupitia Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar ipo mbioni kuanzisha Kituo cha Utatuzi wa Migogoro nje ya Mahkama (ADR Center) pamoja na Sheria zinazosimamia uanzishwaji na uendeshaji wa Kituo hicho.

Kukamilika kwa Kituo hicho kutasaidia kutatuliwa kwa migogoro kwa haraka, na kinatarajiwa kuchochea zaidi ongezeko la Wawekezaji wanaokuja Zanzibar kwa vile Wawekezaji hao watakuwa na amani na uwekezaji wao nchini.

Naibu MWANASHERIA Mkuu ZANZIBAR Shaaban Ramadhan Abdalla ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa kupokea maoni kuhusu Rasimu ya uanzishwaji wa Kituo hicho huko katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi hiyo Mazizini uliohudhuriwa na Wataalam wa Sheria kutoka katika Taasisi za Serikali na binafsi nchini.

Naibu Shaaban amesema Sheria iliopo ya Utatuzi wa Migogoro Sura Nam. 25 ya mwaka 1928 imepitwa na wakati kwa vile ilianzishwa enzi za ukoloni na haiendani na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia ambayo yamefikiwa nchini.

Amesema kulingana na kasi ya ukuaji wa uchumi, teknolojia na shughuli mbali mbali za kiuwekezaji Sheria hiyo inahitaji kuimarishwa zaidi ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo.

“Mambo yatakapokamilika tutaifuta ‘Arbitration decree’ na tutakuja na ‘Arbitration Act’ pamoja na kanuni ambazo zinasaidia kutatua migogoro kwa wakati tulionao” alifafanua Naibu Mwanasheria Mkuu.

Amefahamisha kuwa, katika hali ya kawaida migogoro inapotokea hupelekwa mahkamani lakini kuna baadhi ya migogoro haihitaji kuwa na taratibu nyingi na za muda mrefu kutatuliwa kwake.

Akitolea mfano Naibu Mwanasheria Mkuu amesema “wote ni mashahidi namna Zanzibar ilivyojikita katika maswala ya uwekezaji na ujenzi hasa wa Miundombinu. Kwenye maswala hayo kesi zikipelekwa katika Mahkama za kawaida zitachukua muda mrefu na hivyo kuathiri uekezaji na uchumi wa nchi. Sasa tunapokuwa na ADR Center kesi hizo zitapelekwa huko na kupata suluhu kwa muda mfupi ili kazi ziendelee”.

Kwa upande wake Mrajisi wa Mahkama Zanzibar Valentina Andrew Katema amesema kuanzishwa kwa Kituo cha Utatuzi wa Migogoro nje ya Mahkama ADR Center kutasaidia kutatua migogoro kwa haraka na kuipunguzia mzigo Idara ya Mahkama.

Amebainisha kuwa, utaratibu wa kwenda Mahkamani ni kwenda kupata hukumu kati ya kushinda au kushindwa jambo ambalo wakati mwingine haliachi picha nzuri miongoni mwa walioshitakiana mahkamani.

Mrajis huyo ameongeza kuwa, Watu watakapoamua kwenda kutatua mgogoro wao katika Kituo cha “ADR Center” kuna uwezekano mkubwa wa kubakia katika mahusiano mema kwa vile hakuna kushindwa wala kushinda bali ni kufikia makubaliano ya pande zilizokuwa na mgogoro.

Akizungumzia faida za Kituo hicho Bi Valentine amesema kuwepo kwa ADR Center kutahamasisha shughuli za kiuchumi kwa vile Wawekezaji watakuja kwa wingi wakijua kwamba kuna namna nzuri ya kusuluhisha Migogoro pale inapoibuka.

Amesema ADR Center itawapa utulivu Wawekezaji kuona kwamba, wanayo sehemu nzuri ya kukimbilia pale shughuli za uwekezaji wao zinapoingia katika migogoro na kupata suluhu kinyume na kupelekana mahkamani.

“Wenzetu wawekezaji wanapokuja kitu cha msingi huzingatia sana usalama wa uwekezaji wao na hawapendi kupelekwa mahkamani kutokana na gharama za Mahkama na kuchukuwa muda mrefu sasa ADR Center itawarahisishia kwa vile kunapotokea shida watafika hapo kwa ajili ya kutatua tatizo nje ya Mahkama” Amefahamisha Valentina

Aidha amefafanua kuwa, kupitia wingi wa wawekezaji nchini kutachochea shughuli za kiuchumi na ongezeko la fursa za ajira kwa wananchi.

Kwa upande wake mmoja wa Washauri elekezi Dkt. Fauz Twaib ambaaye ni Jaji Mstaafu na Rais wa Jumuiya cha Wanasheria Afrika Mashariki amesema lengo la kazi wanayoifanya ni kuleta Sheria ambayo itaweka masharti ya jinsi gani Sheria za usuluhishi hasa wa migogoro zinavyotakiwa kufanya kazi Zanzibar kwa zama za sasa.

Amesema kupitia kazi hiyo wanakusudia kuubadilisha mfumo wa Sheria hizo za utatuzi wa migogoro ambao kwa sasa sheria yake ina zaidi ya miaka 100 toka kuanzishwa kwake na kwamba haiendani ten ana hali halisi.

Dkt. Fauz amefahamisha kuwa kazi yao kubwa ni kuandaa sheria mbali mbali hasa Sheria hiyo ya usuluhishi lakini pia wamependekeza kituo maalum kwa ajili ya utatuzi wa Migogoro ingawa haitoshughulika na maswala yote kwa vile migogoro mingine itapelekwa katika Mahkama za kawaida.

Amepongeza maoni yaliyotolewa na na Wadau wa Sheria na kwamba watayachukua na kwenda kuyafanyia kazi ili kuikamilisha Rasimu hiyo ikiwa bora zaidi na kuikabidhi Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar kwa hatua za mbele zaidi.

No comments: