Na Eleuteri Mangi WANMM
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia umeongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi nchini kutoka asilimia 25 hadi 35 hatua inayosaidia kuinua kiuchumi wao na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Mradi LTIP Bw. Joseph Shewiyo unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati akifungua kikao kazi cha Asasi za kiraia kujadili utekelezaji wa mradi huo Januari 16, 2024 jijini Dodoma.
"Mna jukumu kubwa, mnapaswa kuongeza wigo katika kutekeleza majukumu yenu kufanikisha kutoa hati milki za kimila ili kuinua uchumi wa wananchi, mna mchango mkubwa kwa ongezeko la wanawake wanaomiliki ardhi kutoka asilimia 25 hadi 35, mkafanye kazi yenu kwa weledi msiharibu ndoa za watu" amesema Bw. Shewiyo.
Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Benki ya Dunia unalenga kuimarisha mifumo ya utawala wa ardhi, kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa wanaume na wanawake na hivyo kukuza uwekezaji wa ardhi nchini.
Majukumu yanayotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa kupanga, kupima na kumilikisha wananchi ardhi mijini na vijijini, kuboresha mifumo ya usimamizi wa taarifa za ardhi nchini, kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mradi.
Aidha, Asasi za Kiraia katika mradi huo zinajukumu la kutoa elimu kwa Jamii kuhusiana na mradi, kutoa elimu kwa makundi maalumu kama vile wanawake, wazee, watoto na watu wenye ulemavu kuhusu haki zao katika umiliki wa ardhi, kushiriki katika utatuzi wa migogoro ya Ardhi, kutoa ushauri wa namna ya kushugulikiamasuala ya Jamii na mazingira yanahusu mradi, kushirikiana na timu ya mradi katika kuandaa taarifa za utekelezaji wa mradi hususani taarifa za masuala ya mazingira na jamii.
Kwa upande wake Mtaalamu Mkuu wa masuala ya Maendeleo ya Jamii kutoka Benki ya Dunia Bw. Nicholas Soikan amesema kikao kazi hicho kina umuhimu mkubwa kwa Uchumi wa mtu binafsi, familia, jamii na taifa kwa ujumla ili kufikia malengo ya mradi huo.
Bw. Soikan ameongeza kuwa Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania wanatambua umuhimu wa asasi za kiraia na zina nafasi ya kutatua migogoro ya ardhi inayojitokeza wanapoishi ili kutekeleza mradi kwa ufanisi.
Kwa upande wao washiriki wa kikao kazi hicho kutoka asasi za kiraia Bw. Jesta Twimanye kutoka Kahama na Bi Mwajumbe kutoka Mbinga wamesema kuwa wamesema wanaendelea kushirikiana na Serikali katika mradi huo na wanaendelea kutoa elimu juu ya haki ya umiliki wa ardhi kwa wanawake na wanaume na mradi umesaidia kuongeza usalama wa ardhi kwa kutoa hati ya umiliki wa ardhi kwa mume na mke.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na wahamasishaji kutoka asasi za kiraia kutoka Chalinze, Shinyanga, Kahama, Nzega, Kigoma, Mufindi, Mbinga, Songwe, Tanganyika, Maswa, Chamwino, Kaliua, Uyuwi, Nkasi, Chunya, Ludewa, Mkakete, Mvomero, Kilwa, Ruangwa, Kilindi, Mkinga, Handeni, Ngara, Rorya, Iramba na Songea.
No comments:
Post a Comment